Biden ataja sharti la kuiruhusu Ukraine kuwashambulia wanajeshi wa Korea Kaskazini

Rais Joe Biden wa Marekani amesema, vikosi vya Ukraine vinapaswa kuwashambulia wanajeshi wa Korea Kaskazini ikiwa watavuka mpaka na kuingia kwenye ardhi ya Ukraine.

Biden ameeleza hayo kufuatia madai kwamba Pyongyang imepeleka askari wake wakapigane bega kwa bega na wanajeshi wa Russia katika vita dhidi ya Ukraine.

Wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon ilidai wiki hii kwamba wanajeshi 10,000 kutoka Korea Kaskazini wamewasili Russia.

Inadaiwa kuwa, baadhi ya askari hao wamesafirishwa kwa ajili ya uwezekano wa kutumwa kwenda kupambana na wanajeshi wa Ukraine katika Mkoa wa Kursk wa Russia, ambapo baadhi ya vikosi vya Kiev vimesalia huko baada ya kulivamia eneo hilo mnamo mwezi Agosti.

Alipoulizwa na vyombo vya habari kama Kiev inapaswa “kujibu mapigo” dhidi ya wanajeshi wa Korea Kaskazini, Biden amejibu kwa kusema: “Ikiwa watavuka na kuingia Ukraine, ndiyo.” Hata hivyo hakufafanua msimamo wa Marekani, kama wanajeshi wa Ukraine waendelee kubaki katika mkoa wa Kursk ambao Washington inautambua kama eneo la ardhi ya Russia.

Moscow na Pyongyang zilitia saini mkataba wa pande mbili mapema mwaka huu ambao unaruhusu kutoa msaada wa kijeshi pale moja kati ya nchi hizo mbili inaposhambuliwa na upande wa tatu.

Rais Vladimir Putin wa Russia amekataa kuthibitisha au kukanusha taarifa za kuwepo wanajeshi wa Korea Kaskazini nchini Russia. Katika mahojiano aliyofanyiwa wiki iliyopita, Putin alisema, kile mataifa hayo mawili yanafanya kutimiza wajibu wao chini ya makubaliano hayo mapya ni suala linalozihusu nchi hizo tu…/