Rais Joe Biden wa Marekani ameripotiwa kuidhinisha Ukraine kutumia makombora ya masafa marefu ya Kimarekani kulenga shabaha ndani ya mipaka ya Russia ya kabla ya 2014.
Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya jana Jumapili iliyotolewa na gazeti la New York Times likiwanukuu maafisa wa Marekani ambao hawakutaka kutajwa majina yao.
Uamuzi huo, ikiwa utathibitishwa kuwa umepitishwa, utaashiria mabadiliko makubwa katika sera za Washington na utashadidisha mzozo wa vita kati ya Moscow na Kiev.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Ukraine inatarajiwa kutumia Mifumo ya Kijeshi ya Makombora ya Kitaktiki (ATACMS) dhidi ya vikosi vya Russia na wanaodaiwa kuwa wanajeshi wa Korea Kaskazini katika Mkoa wa Kursk nchini Russia, ambako mapigano makali yangali yanaendelea.
Kuwepo kwa vikosi vya Korea Kaskazini kumetumika kama sehemu ya uhalalishaji wa mabadiliko ya sera za Washington, ingawa hakuna uthibitisho kwamba wanajeshi wa Pyongyang wanahudumu kijeshi nchini Russia.

Hapo awali, Marekani ilipinga Ukraine kutumia makombora hayo ya ATACMS ya masafa marefu dhidi ya Russia, ikitaja wasiwasi juu ya uwezekano wa kulipiza kisasi Kremlin.
Makombora hayo yanayofika umbali wa kilomita 300 (maili 186) na ambayo usahihi wake unaongozwa na GPS, hutoa nguvu kubwa ya moto.
Ikulu ya Russia, Kremlin bado haijatoa kauli yoyote juu ya suala hilo.
Biden anaripotiwa kuchukua msimamo wa kuidhinisha Ukraine kutumia makombora ya masafa marefu dhidi ya Rusia wakati mrithi wake katika Ikulu ya White House, rais wa zamani Donald Trump, ameashiria uwezekano wa kukatisha kutoa misaada zaidi ya kijeshi kwa Ukraine na kuiacha katika hali mbaya ya kuweza kuendelea kupambana kivita na Moscow.
Trump ameahidi pia kuhitimisha haraka vita hivyo, ingawa hajajulikana ni njia gani ataweza kutumia kufanya hivyo…/