‘Biashara United’ ya England yaitupa nje Liverpool FA

Plymouth. Mdharau mwiba mguu huota tende! Ndio kauli ambayo uhalisia wake umeonekana jana Februari 9, 2025 baada ya vinara wa Ligi Kuu England (EPL), Liverpool kutupwa nje ya Kombe la FA baada ya kupokea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Plymouth inayoshika mkia katika Ligi Daraja la Kwanza England (Championship) ikifanana na Biashara United ya Mara inayoshika mkia katika Ligi ya Championship kwa huku Tanzania.

Kujiamini kwa meneja wa Liverpool, Arne Slot hado kufikia kupumzisha wachezaji 10 tegemeo wa kikosi cha kwanza kulikuwa na faida kwa Plymouth ambayo ilihitaji shuti moja tu kati ya mawili iliyopiga kwenye mchezo mzima, kupata bao ambalo limeivusha kwenda raundi ya 16 bora ya mashindano hayo.

Wachezaji 10 wa Liverpool waliokosena kwenye mchezo huo wa jana ni Virgil van Dijk, Mohamed Salah, Alisson, Ibrahima Konate, Alexis Mac Allister, Ryan Gravenberch, Dominik Szoboszlai, Cody Gakpo, Conor Bradley na Andy Robertson.

Hata hivyo kocha huyo aliwapanga baadhi ya wachezaji wazoefu kikosini kama vile Luis Diaz, Jota, Federico Chiesa, Elliott, Wataru Endo na Kostas Tsimikas.

Bao pekee la Plymouth ambalo limeizamisha Liverpool katika mchezo wa jana lilifungwa na Ryan Hardie kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 53n ambayo timun yake ilipata baada ya Harvey Elliott kunawa mpira ndani ya eneo la hataru.

Pamoja na kutolewa, Slot ametamba kuwa amefanya kitu sahihi na kutolewa ni jambo la kawaida.

“Leo nadhani tumeonyesha kwa nini tumewatumia hawa wachezaji kwa sababu wachezaji hawa wanahitaji kuendana na kasi ya mchezo katika miezi ijayo.Wanahitaji muda wa kucheza na unaona baadhi ya wachezaji wanahitajika kuwa kama hivi,” alisema Slot.

Hata hivyo pamoja na kutolewa, ndoto ya Liverpool kutwaa mataji matatu kwa mpigo msimu huu bado ipo hai kwani imeingia fainali ya Kombe la Carabao, imetinga hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na inaongza msimamo wa Ligi Kuu England ikiwa na pointi 56.

Kwa upande mwingine kutolewa na Plymouth kumeua ndoto ya Liverpool kutwaa taji hilo kwa mara ya tisa.

Timu zilizofanikiwa kutinga raundi ya tano ni;

  • Manchester United
  • Millwall
  • Brighton & Hove Albion
  • Preston North End
  • Ipswich Town
  • Fulham
  • Newcastle United
  • Plymouth Argyle
  • AFC Bournemouth
  • Aston Villa
  • Burnley
  • Manchester City
  • Doncaster Rovers or Crystal Palace
  • Cardiff City.