Besigye kuendelea kushikiliwa mahabusu Mahakama ikiahirisha kesi

Kampala. Kiongozi wa upinzani anayeugua nchini Uganda, Dk Kizza Besigye, msaidizi wake Obeid Lutale na mmoja wa mawakili wao watasalia kizuizini hadi baadaye mwezi huu wakati Mahakama Kuu ya Kampala itakapotoa uamuzi wake katika kesi ya kutaka watuhumiwa hao wafikishwe mahakamani, iliyowasilishwa na mawakili wao.

Baada ya kusikiliza mawasilisho, hakimu wa Mahakama Kuu, Douglas Karekona Singiza alisema Jumatano kwamba uamuzi wake utatolewa kabla ya Februari 25, 2025.

“Viongozi wa magereza wanapaswa kuwachukua tena Kanali Kizza Besigye na Obeid Lutale na kubaki na mawakili na kuendelea na ombi la kutaka wafikishwe mahakamani,” Dk Singiza alisema wakati wa shauri hilo huku akipuuza maombi ya mawakili wa Dk Besigye ya kutoa amri ya muda wa kuachiliwa kwa mgombea huyo wa urais mara nne kutafuta huduma bora za afya nje ya gereza la Luzira ambako amekuwa akizuiliwa tangu Novemba mwaka jana.

Jaji huyo alisema anafurahi kwamba angalau mwili wa Dk Besigye umewasilishwa mahakamani na sasa kilichobaki ni maswali kuhusu kuzuiliwa kwake kinyume cha sheria kufuatia Serikali kuchelewa kutekeleza uamuzi wa Mahakama ya Juu wa Januari 31 ambao ulisimamisha Mahakama Kuu ya kijeshi kuwahukumu raia kwa madai kuwa ni kinyume cha katiba kabla ya kuamuru faili kuhamishiwa mara moja katika mahakama za kawaida zenye mamlaka.

Dk Besigye alikuwa akitaka kuachiliwa kutoka kifungoni, saa chache baada ya Chama cha Wanasheria wa Uganda (ULS) kuandika barua, Jumatatu iliyopita, kupinga kucheleweshwa kusikilizwa kwa ombi la Jaji Douglas Karekona Singiza.

Lakini saa chache baada ya uamuzi wa mahakama, mke wa Dk Besigye, Winnie Byanyima na Rais wa Jukwaa la Umoja wa Kitaifa (NUP), Robert Kyagulanyi, almaarufu Bobi Wine, walielezea kuendelea kuzuiliwa kwake na maagizo ya jaji kama mateso ya kisiasa.

“Jaji na utawala wanamtesa Dk Kizza Besigye na wafungwa wengine wa kisiasa kwa jina la mashtaka. Wito wangu pekee kwa Waganda wa hapa na nje ya nchi, ni kuendelea kutoa shinikizo. Hatutaacha. Tuliupa utawala saa 48 kumwachilia Dk Besigye kwa sababu tunamtaka akiwa hai. Wanajaribu kumuua,” alisema Wine.

Kwa upande wake, Byanyima alisema amesikitishwa na mahakama kushindwa kumuachia mume wake kutafuta huduma bora za matibabu.

“Nilikuja hapa nikitarajia kumrudisha nyumbani leo. Nimeumia sana lakini sishangai. Besigye ni mfungwa. Alitekwa nyara na yuko kifungoni kama sisi sote. Museveni ametuweka wote kifungoni. Aibu kwa jaji huyu kwa kumrudisha mume wangu jela wakati afya yake inazidi kuzorota,” alisema.

Hivi karibuni, afya ya Dk Besigye imezorota, ikiripotiwa kutokana na mgomo wa kutokula kwa muda mrefu. Jumapili iliyopita, alipelekwa katika zahanati binafsi huko Bugolobi kwa vipimo vya afya. Baadaye alirudishwa jela.