
MAMBO yameanza kuchangamka baada ya RS Berkane ya Morocco itakayocheza na Simba katika mechi mbili za fainali za Kombe la Shirikisho Afrika kudaiwa kutuma watu wanne ili kuja nchini kuisoma ikila viporo vya Ligi Kuu Bara, ambapo leo jioni itaumana na Pamba Jiji, Uwanja wa KMC.
Simba itaanzia ugenini kuvaana na Berkane Mei 17 kabla ya kurudiana nao Kwa Mkapa Mei 25 kombe likiwa uwanjani, huku taarifa zikisema tayari Wamorocco wametuma mashushushu wanne ili kuipeleleza vya kutosha Simba katika mechi za ligi kabla ya kuwasubiri kwa fainali ya kwanza ugenini.
Simba imetinga fainali kwa kuing’oa Stellenbosch ya Afrika Kusini kwa ushindi wa jumla wa bao 1-0 wakati wapinzani wake waliitoa CS Constantine ya Algeria kwa jumla ya mabao 4-1, na katika kuhakikisha wanaisoma kwa undani Berkane imetuma mashushushu hao wanne akiwemo mtathmini wa mechi kupitia video (video analyst).