Benki yakomalia ushiriki matukio ya mbio kuboresha afya, utalii

Dar es Salaam. Ili kukuza chachu ya ufanyaji mazoezi, mshikamano na uzalendo wa kitaifa Benki ya Absa Tanzania imesisitiza jamii katika ushiriki wa mbio za Absa Dar City Marathon 2025 zenye faida ikiwemo kiafya, misaada na utalii.

Mbio hizo zinatajwa kuwa zaidi ya ufanisi wa wanariadha zikiwa na lengo la kukuza afya ya jamii kama anavyosema Beda Biswalo, Meneja wa chapa na Mawasiliano wa Benki ya Absa Tanzania alipokuwa akizungumza baada ya mbio hizo zilizofanyika Jumapili Mei 4, 2025 jijini hapa.

Biswalo amesema mbio hizo zinaendana na lengo lao la kuhamasisha maisha yenye afya, kukuza mwingiliano wa kijamii na kuchangia maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Katika mbio hizo za Absa Dar City Marathon 2025 zaidi ya wakimbiaji 3,500 wajitokeza ikiwa idadi hiyo imepanda kutoka washiriki 2,500 mwaka jana, ikionyesha ni kwa namna gani  mbio hizo zimeendelea kuvutia umma na kuchangia katika michezo, jamii na sekta ya utalii nchini.

“Kwa kuendeleza lengo la kusaidia jamii, sehemu ya ada za usajili wa mwaka huu itaelekezwa kusaidia wodi ya wazazi katika Hospitali ya Mnazi Mmoja.”

“Kama sehemu ya shughuli za baada ya mbio, Absa inapanga kuendesha shughuli ya uchangiaji damu kwa ajili ya benki ya Taifa ya damu jambo linaloonyesha wazi dhamira ya mashindano haya kutoa mchango kwa jiji na wakazi wake,” amesema Biswalo.

Aidha, mbio hizo ambazo huandaliwa na The Runners Club kwa udhamini wa Benki ya Absa Tanzania, sasa zimejikita kama tukio la kila mwaka la mbio katikati ya jiji zikiwa na ndoto ya kuwa tukio kubwa zaidi la riadha siyo tu Tanzania bali pia Afrika Mashariki.

Katika mbio hizo washiriki walichuana katika viwango vitatu: kilomita 5, kilomita 10 na nusu marathon ya kilomita 21, huku mipango ikiendelea kupanua zaidi tukio hili.

“Kwetu Absa, tunaamini hadithi yako ni muhimu. Huu siyo msemo tu bali ni dhamira yetu ya kutembea bega kwa bega na Watanzania wanapoandika sura mpya zenye hamasa katika maisha yao.

“Afya bora ni msingi wa maisha yenye maana, na marathon hii ni sehemu yetu ya kusaidia maelfu kuanza au kuendeleza safari hiyo,” amesema Aron Luhanga, Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Absa Bank Tanzania.

Tukio hilo linamuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan, katika jitihada zake za kuitangaza Tanzania kama kivutio cha utalii. Washiriki kutoka nje ya nchi wanatarajiwa kuongezeka katika matoleo yajayo, hivyo kuiweka Dar es Salaam kwenye ramani ya dunia ya mashindano ya mbio.

Toleo la mwaka huu pia lilitambua vipaji vya kipekee kwa kuwatuza washindi wa kila kundi kwa zawadi mbalimbali ikiwa ni pamoja na vikombe, zawadi ya fedha taslimu na vifaa vya michezo vyenye nembo ya Absa.

Benki ya Absa Tanzania kwa kushirikiana na The Runners Club tayari wameanza maandalizi ya Absa Dar City Marathon 2026, wakiwa na matarajio ya kupanua zaidi tukio hilo, kuongeza ubunifu na kushirikisha wakimbiaji kutoka ndani na nje ya Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *