
Dar es Salaam. Benki ya NCBA Tanzania imeendelea kuonesha dhamira yake ya kuimarisha ujumuishaji wa kifedha na mahusiano ya kijamii kupitia hafla maalum ya Iftar ya Ramadhani iliyoandaliwa katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam.
Hafla hiyo iliyofanyika jana Machi 27, 2025 iliwakutanisha wadau wakuu wa sekta ya benki, wateja, na viongozi wa dini kwa lengo la kusherehekea mwezi mtukufu wa Ramadhani huku benki hiyo ikiangazia mchango wake katika sekta ya kifedha nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa NCBA, Claver Serumaga, alisema benki hiyo inaendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha kupitia benki za kidijitali na suluhisho za kifedha zinazotegemea teknolojia ya simu za mkononi.
“Ujumuishaji wa kifedha ni nyenzo muhimu katika kuwezesha maendeleo ya kiuchumi. NCBA inaendelea kuhakikisha kila Mtanzania, bila kujali mahali alipo, anapata huduma bora za kifedha kupitia mifumo ya kidijitali,” alisema Serumaga.
Aliainisha kuwa majukwaa ya M-Pawa na NCBA Now yamekuwa chachu ya mageuzi katika sekta ya benki nchini kwa kurahisisha huduma kama uwekaji wa akiba, upatikanaji wa mikopo, na usimamizi wa fedha kwa njia ya mtandao.
Naibu Kadhi wa Tanzania, Sheikh Ally Hamisi Ngeruko, ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliipongeza NCBA kwa juhudi zake katika kusaidia jamii ya Kiislamu na kukuza ujumuishaji wa kifedha.
“Ramadhani ni kipindi cha mshikamano na kusaidiana. NCBA imeonesha kujali jamii kwa kutoa suluhisho za kifedha zinazorahisisha maisha ya Watanzania, hususan kwa wajasiriamali wadogo na biashara ndogo na za kati,” alisema Sheikh Ngeruko.
Kwa mujibu wa NCBA, huduma za kifedha za kidijitali zinaendelea kubadilisha jinsi wateja wanavyoshirikiana na fedha zao. Kupitia NCBA Now, wateja wanaweza kufanya miamala, kulipa bili, na kupata huduma za kifedha papo hapo kwa kutumia simu zao za mkononi.
Huduma ya M-Pawa, inayotolewa kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania, inatoa fursa kwa wateja kuweka akiba kwa usalama na kukopa papo hapo, hivyo kuwawezesha kusimamia mahitaji yao ya kifedha kwa ufanisi.
NCBA pia imeeleza kuwa inazidi kuwekeza katika suluhisho maalum kwa biashara ndogo na za kati (SMEs), zikiwemo mikopo ya mtaji wa kazi na ufadhili wa ununuzi wa vifaa vya biashara. Huduma hizi zinalenga kusaidia biashara kupanuka na kuwa endelevu.
Aidha mbali na huduma za kifedha, NCBA imeendelea kushiriki katika miradi ya maendeleo ya jamii. Mapema mwaka huu, benki hiyo ilifanya kampeni ya upandaji miti 6,000 katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni sehemu ya mpango wake wa uendelevu wa mazingira.
Kwa kuwa sekta ya kifedha inaendelea kukumbatia teknolojia, NCBA inajipanga kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma bora za kidijitali, kusaidia biashara ndogo na za kati, na kushiriki katika maendeleo ya kijamii nchini Tanzania.