Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa kushirikiana na kampuni ya Mbogo Ranches wamezindua rasmi mpango wa utoaji wa mikopo rafiki kwa wafugaji kwa ajili ya ununuzi wa mbegu bora na za kisasa za mifugo.
Makubaliano haya yaliyosainiwa katika Maonesho ya Mifugo ya Kimataifa ya Mbogo 2025 yanatoa fursa kwa wafugaji kupata ng’ombe, mbuzi, na kondoo bora kwa masharti nafuu ya mkopo kupitia benki hiyo, hatua inayolenga kuchochea maendeleo ya sekta ya mifugo nchini.
Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi wa Idara ya Wateja Wadogo na Wakubwa wa NBC, Elibariki Masuke amesema mpango huo ni sehemu ya juhudi za benki hiyo katika kuimarisha uchumi jumuishi kupitia huduma rasmi za kifedha. Alifafanua kuwa wafugaji watakaovutiwa na mbegu yoyote kutoka Mbogo Ranches watawezeshwa kupata mkopo kupitia matawi ya NBC kwa masharti ya kulipa kidogo kidogo kwa bei ile ile ya shambani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mbogo Ranches Naweed Mulla amesema mpango huo ni suluhisho kwa wafugaji waliokuwa wakishindwa kumudu gharama kubwa za mbegu hizo bora kutokana na changamoto za gharama za uzalishaji na uingizaji wa mifugo kutoka nje ya nchi. Alieleza kuwa kupitia ushirikiano huu, wafugaji wengi sasa wataweza kubadili mbegu za asili zisizozalisha kwa tija na kutumia mbegu bora zinazozalisha kwa ufanisi mkubwa.
Mulla alitoa wito kwa wafugaji kuanza kurasimisha shughuli zao ikiwa ni pamoja na kufungua akaunti rasmi za benki, kupata TIN number na kujiandikisha kisheria ili kufikia fursa kama hizi kwa urahisi. Alisisitiza kuwa urasimishaji wa shughuli za ufugaji ni hatua muhimu kuelekea ufugaji wa kisasa unaohitaji mbinu na miundombinu rasmi ya kifedha na kibiashara.
#AzamTVUpdates
Mhariri | John Mbalamwezi