Benki ya CRDB katika nyayo za mafanikio ya Serikali ya Rais Samia

Dar es Salaam. Katika kitabu cha safari ya mafanikio ya Dk Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benki ya CRDB inazo kurasa zake za kutosha.

Katika miaka minne ya uongozi wa Rais Samia, Benki ya CRDB imeshuhudia kukua kwa faida na ongezeko la thamani ya mali zake mwaka hadi mwaka pamoja na kupanda kwa kodi inayolipa hivyo kuwa sehemu muhimu ya mipango ya Serikali inayolenga kukuza uchumi wa nchi na kuimarisha kipato cha wananchi wake.

Wakati Taifa likisherehekea mafanikio ya uongozi wa Rais Samia kwa miaka minne madarakani, kuna namna Benki ya CRDB imenufaika na mazingira mazuri ya kibiashara yaliyokuwapo katika kipindi hicho yaliyoiruhusu nayo kukua na kuchangia zaidi maendeleo ya Watanzania na uchumi wa Taifa.

Muonekano wa madarasa yaliyojengwa na Benki ya CRDB katika Shule ya Msingi ya Support Union iliyopo Wilaya ya Babati, mkoani Manyara.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela anasema benki imeimarika katika maeneo tofauti kuanzia ukubwa wa mizania yake, mikopo inayotoa hata amana za wateja inazopokea jambo linaloiwezesha kurudisha pa kubwa zaidi kwa wananchi inaowahudumia.

Nsekela anasema mbali na kutekeleza sera yao inayotaka kutengwa kwa asilimia moja ya faida inayopatikana kila mwaka kwa ajili ya kuwezesha miradi ya kijamii, Benki ya CRDB imeendelea kuimarisha biashara zake na kujisogeza jirani zaidi na wananchi kupitia taasisi yake ya CRDB Bank Foundation.

“Kupitia sera yetu ya uwekezaji kwenye jamii pamoja na taasisi yetu ya CRDB Bank Foundation tunayo maeneo manne ya kipaumbele ambayo ni elimu, afya, mazingira pamoja na uwezeshaji wa wanawake na vijana. Ndani ya miaka minne ya uongozi wa Rais Samia, tumeyagusa maeneo haya na kupeleka tabasamu kwa watu tulioshirikiana nao,” anasema Nsekela.

Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB Bank Foundation, Martin Warioba (katikati), na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa (kulia kwake) wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa biashara changa za vijana waliokabidhiwa mitaji wezeshi ya jumla ya Sh 236.57 milioni kupitia programu ya Imbeju.

Kuimarika kwa biashara ya kipindi hiki ambacho Benki ya CRDB imeshuhudia ufanisi mkubwa katika maeneo tofauti, Nsekela anasema kunatokana na uongozi wenye maono wa Rais Samia ambaye misimamo yake katika uchumi ni kukuza kipato na kufungua fursa nyingi zaidi kwa wananchi.

“Juhudi za Rais katika kuboresha maisha ya wananchi kwa kuhamasisha matumizi ya nishati safi, kuimarisha miundombinu ya usafiri, kuhamasisha utalii na mambo mengine mengi anayoyafanya, kunafungua fursa kwa wananchi na kuongeza mapato kwa wafanyabiashara. Mapato yakiongezeka faida nayo inapanda hivyo kutuwezesha kufanya mambo mengi zaidi,” anasema Nsekela.

Mchango katika sekta ya elimu

Benki ya CRDB imekuwa ikitekeleza miradi kadhaa inayoibuliwa na wananchi katika kuimarisha elimu na mazingira ya kujifunzia nchini. Mchango wa Benki ya CRDB katika elimu umekuwa ukijielekeza katika kujenga madarasa, vyoo, ofisi za walimu, mabweni na kununua madawati, viti, meza, kompyuta na mahitaji mengine muhimu.

Ili kuongeza tija katika kufanikisha miradi ya elimu, Benki ilizindua Programu ya Keti Jifunze inayolenga kusaidia kutengeneza madawati, viti, kujenga madarasa, mabweni na ofisi kote nchini.

Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Benki ya CRDB, Tully Mwambapa anasema kwa mwaka 2024, benki imetumia zaidi ya shilingi bilioni 2.31 katika miradi ya uwekezaji kwa jamii.

Muonekano wa wodi iliyokarabatiwa na Benki ya CRDB wikayani Bagamoyo mkoani Pwani.

Katika kiasi hicho, anasema shilingi bilioni 1 ambazo ni sawa na asilimia 44 zimeelekezwa kwenye sekta ya elimu zikitumika kujenga vyumba vya madarasa na vyoo katika shule zilizopo wilayani Babati, Kondoa, Nyamagana, na Muheza.

Shilingi milioni 156 zimetumika kufadhili miradi ya afya huku shilingi milioni 432 zikitumika kuwawezesha wanawake na vijana wajasiriamali na shilingi milioni 281.3 zikielekezwa kwenye miradi ya kulinda na kutunza mazingira. Benki pia ilitumia shilingi milioni 438 kufanikisha miradi mingine ya kijamii.

Fedha zilizotengwa kwa ajili ya elimu, zimetumika kutengeneza madawati, viti na meza pamoja na kununua kompyuta zinazotumiwa na maelfu ya wanafunzi nchini.

“Mwaka 2024 tulielekeza nguvu na kuwafikia wanafunzi wenye mahitaji maalumu ili kuboresha mazingira yao ya kujifunza. Tulijenga madarasa yanayofikika kirahisi na wanafunzi hao, tukatengeneza madawati, viti pamoja na meza kwa ajili yao na kuwapa mahitaji mengine muhimu yakiwamo magodoro katika shule zilizopo katika mikoa ya Rukwa, Manyara na Songwe,” amesema Tully.

Kwa mwaka 2024 pekee, Programu ya Keti Jifunze imetumia zaidi ya shilingi milioni 350 kutengeneza madawati 1,600 pamoja na viti na meza 1,595 vilivyosambazwa katika shule 57 zilizopo katika halmashauri 53 nchini.

Mchango katika sekta ya afya

Afya ni kipaumbele cha kila mtu, familia na Taifa pia kwani ni kwa kuwa na afya njema tu ndipo jamii inaweza kutekeleza mipango yake. Benki ya CRDB inaamini afya ni mtaji wa msingi kwa maendeleo ya biashara za wateja wake ndio maana wakati wote inashiriki kutatua changamoto zinazojitokeza katika jamii.

Meneja wa Benki ya CRDB, Kanda ya Kusini, Denis Mwokela (kushoto) akikabidhi madawati kwa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Liwale, Damas Mumwi (kulia) kwa ajili ya Shule ya Sekondari Nangando iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Liwale, mkoani Lindi.

Katika eneo hili, Benki ya CRDB imekuwa ikishiriki kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya, kutoa elimu ya afya ili kuongeza uelewa kwa wananchi, na kutatua changamoto zinazochelewesha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi kwa kujenga wodi, kutoa vifaatiba na nyenzo nyingine muhimu.

Benki hutekeleza haya yote kwa kushirikiana na wadau kama vile Programu ya Afya Cheki, Ali Kimara Rare Diseas-es Foundation, na halmashauri zote nchini.

Kupitia Mbio zake za Hisani za CRDB (CRDB Bank Marathon), Benki ya CRDB imekuwa ikitenga fedha zote zinazopatikana kwa ajili ya kusaidia matibabu ya watoto wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), kujenga kituo cha miito katika Taasisi ya Saratani Ocean Road na kufanikisha matibabu ya wanawake wenye ujauzito hatarishi wanaotibiwa katika Hospitali ya CCBRT.

Peter Dyaro, mzazi wa moja ya watoto waliokuwa na changamoto ya moyo na kutibiwa, anasema: “Mwanangu alikuwa akipata maumivu makubwa na niliambiwa gharama za upasuaji ni kuanzia shilingi milioni 5 mpaka shilingi milioni 30, pesa ambayo sikuwa nayo. Niliposikia habari za mpango wa Benki ya CRDB ilinibidi nisafiri kutoka Hanang mpaka Dar es Salaam kumleta atibiwe. Na namshukuru Mungu, mwanangu amepona kupitia wao.”

Utunzaji wa mazingira

Kwa kufahamu ukubwa wa athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi, Benki ya CRDB imelipa uzito mkubwa suala hili hivyo kushiriki kikamilifu katika mipango ya kulinda mazingira.

Mwaka 2019, benki ilianzisha kampeni ya kitaifa ya upandaji miti inayojulikana kama “Pendezesha Tanzania” kwa lengo kutunza mazingira. Zaidi ya miti 12,000 imeshapandwa mpaka sasa hivyo kusaidia kulinda vyanzo vya maji, kuihamasisha jamii kupanda miti na kulinda mazingira pamoja na kuongeza uelewa juu ya umuhimu wa kulinda mazingira.

Ili kuishirikisha jamii kwa ukubwa zaidi, mwaka 2023 Benki ya CRDB ilizindua Hatifungani ya Kijani yenye lengo la kusaidia ufadhili wa miradi yenye mrengo wa kulinda na kuboresha mazingira nchini.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima akikabidhi mfano wa hundi kwa kikundi cha wanawake wajasiriamali waliokidhi vigezo vya kupata mtaji wezeshi kutoka CRDB Bank Foudation kwenye Maonesho ya Imbeju ya Wajasiriamali Ilala.

Kupitia hatifungani hiyo, benki ilikusanya shilingi bilioni 171.82 ambazo tayari zaidi ya shilingi bilioni 88.5 zimekopeshwa kwenye miradi ya nishati jadidifu, kilimo kinacholinda mazingira, majengo yanayolinda mazingira, usafirishaji, maji, na usafishaji wa maji.

Benki ya CRDB pia inasaidia utekelezaji wa mikakati ya Serikali ya kulinda mazingira ikiwamo kampeni ya nishati safi ya kupikia inayotekelezwa na Wizara ya Nishati pamoja na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kwa kuwawezesha wananchi kupata mitungi ya gesi ya kupikia.

Vilevile, Benki kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ilinunua kilo 7,142 za mbegu za mahindi zenye thamani ya shilingi milioni 50 kwa ajili ya kuwawezesha waathirika wa mafuriko yaliyotokea wilayani Rufiji kuendelea na kilimo baada ya mazao yao kusombwa na mafuriko yaliyotokea mwaka jana.

Uwezeshaji vijana na wanawake

Ndani ya miaka minne ya uongozi wa Rais Samia, Benki ya CRDB imepiga hatua kubwa ikiwamo kuanzisha kampuni tanzu ya CRDB Bank Foundation inayotekeleza Programu ya Imbeju iliyojikita katika kuwawezesha wanawake, vijana na makundi maalumu.

Kuanzishwa kwa CRDB Bank Foundation mwaka 2023 kulienda sambamba na kuzinduliwa kwa Programu ya Imbeju inayotoa mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya fedha, pamoja na kuwapa wahusika mitaji wezeshi ya kukuza na kuimarisha biashara zao.

Washiriki waliohudhuria semina za Imbeju wamenufaika kwa elimu ya fedha na mafunzo ya ujasiriamali yatakayowawezesha kukuza biashara zao. Hadi Januari 2025, CRDB Bank Foundation ilikuwa imetoa elimu ya fedha na mafunzo ya biashara kwa zaidi ya wanawake na vijana wajasiriamali 800,000.

“Kwa kipindi hiki chote, tumetoa mitaji wezeshi yenye jumla ya thamani ya shilingi bilioni 20.2,” anasema Tully. Ili kuhakikisha vijana wanashiriki shughuli za kiuchumi huku wakiimarisha afya zao, Benki ya CRDB inadhamini ligi za michezo mbalimbali ili kutoa fursa kwa kila mmoja kupata nafasi.

Benki ya CRDB ndio mdhamini wa Ligi ya Shirikisho inayovihusisha kuanzia vilabu vya daraja la tatu mpaka Ligi Kuu. Vilevile, inadhamini mashindano ya mpira wa kikapu ya CRDB Bank Taifa Cup.

Pia, benki hiyo imekuwa mdhamini wa mashindano ya mbio za ngalawa kule Kizimkazi Zanzibar kwa miaka kadhaa sasa. Programu nyingine ambazo Benki ya CRDB inaziwezesha ni pamoja na Malkia wa Nguvu ya Clouds Media Group, Kizimkazi Festival kule visiwani Zanzibar.

Kwa jinsi Serikali inavyoendelea kuweka mazingira rafiki ya ufanyaji biashara, Benki ya CRDB inaamini itaendelea kuimarika na kutanuka zaidi ndani na nje ya nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *