
KOCHA wa zamani Simba, Abdelhak Benchikha, ambaye yupo nchini Misri akiifundisha Modern Sport,amewapa Simba mbinu tatu za haraka za kuwakabili Al Masry ya kupata matokeo Jumatano.
Simba chini ya Kocha Fadlu Davids itakuwa na kibarua cha kuanzia ugenini Aprili 2, dhidi ya Al Masry ya Misri, ikiwa ni mchezo wa kwanza hatua ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho Afrika.
Wapinzani hao wa Simba ambao wanashika nafasi ya nne katika ligi ya Misri. Lakini kwa mujibu wa mahojiano ya Mwanaspoti na Benchikha, Mnyama anapaswa kufanya mambo matatu ya msingi sana kama anataka kumaliza mchezo mapema.
Kwanza kuhakikisha wanakuwa imara kwenye safu yao ya ulinzi ndani ya dakika 20 za mwanzo bila kuruhusu makosa yoyote huku wakiongeza umakini kwenye mipira yote ya krosi inayopigwa dhidi yao kwani Waarabu hao ni wajanja.
Lakini pili wanapaswa kuwatibua wasimiliki sana mpira kwa kujiimarisha kwenye kiungo muda wote na mwisho kwenye ushambuliaji mastraika wa Simba wasifanye kosa kwa kudhani watapata nafasi tatu za kujaribu kubahatisha goli kwa Al Masry. Akimaanisha kwamba kila sekunde wanayoipata mbele ya kipa Mahmoud Gad, raia wa Misri.
Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu akiwa Misri alisema; “Lazima wawe imara kwenye ulinzi haswa dakika 20 za kwanza ambazo wenyeji wao huwa wanatafuta bao kwa nguvu ili wamiliki mchezo.
“Hapo ni lazima kocha wa Simba apange safu yake ya kiungo imara, lakini pia ukuta wake ujue kucheza krosi na wasiruhusu sana wapinzani wao, wawashambulie ndani ya eneo la hatari.
“Taarifa mbaya kwa Simba kumkosa Che Malone, ni beki mzuri mwenye uzoefu, lakini watakaocheza wapunguze makosa na akili zao wakati wote ziwe uwanjani.
“Safu ya ushambuliaji lazima iwe na haraka kuwaadhibu Al Masry, wanapofanya makosa kwani haiwezi kuwa nayo mengi hasa kwenye ulinzi lakini yatatokea, washambuliaji wa Simba hawatakiwi kusubiri nafasi tatu ili wafunge,” alisema Benchikha.
Rekodi za Al Masry katika ligi ya ndani zinaonyesha kuwa mchezo wa mwisho walitoka sare 1-1 na timu ya National Bank of Egypt na kuwafunga dakika ya 15 kipindi cha kwanza.
Ilitokea kundi D ikimaliza nafasi ya pili ikifunga mabao saba na kuruhusu manne, ikikusanya jumla ya pointi tisa kwenye kundi lililoongozwa na ndugu zao Zamalek wakiwa na pointi 14.
Kwenye mechi hizo sita za makundi Masry, ilishinda mechi mbili tena zote za nyumbani dhidi ya Black Bulls ya Msumbiji (3-1) na Enyimba ya Nigeria (2-0) kisha ikatoa sare tatu na kupoteza mmoja dhidi ya Zamalek (1-0), ikionyesha kuwa ni timu imara.
Mshambuliaji Ben Youssef ambaye kwenye mechi za makundi, alimaliza na mabao matatu aliyopiga Hat Trick kwenye mchezo wa ushindi dhidi ya Black Bulls ndiye tegemeo lao. Alijumuishwa kwenye kikosi Bora cha mechi za makundi kilichotolewa na CAF, sambamba na huyo Hamada Mahmoud aliyemaliza na mabao mawili, Mido Gaber na Mohammed Hashem.
KWENYE LIGI ZAO
Al Masry ni ya nne kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 31, ambazo ni pointi 12 pungufu ya za vinara Pyramids wenye pointi 43, huku Simba ikiwa ya pili kwa pointi 57, moja nyuma ya Yanga.
Katika mechi tano zilizopita kwenye mashindano yote Al Masry wamelazimishwa sare tatu, kushinda moja na kupoteza moja.
Lakini Simba, katika mechi tano imeshinda nne kwa idadi kubwa ya mabao na sare moja ya 2-2 dhidi ya Azam FC.