
BEKI wa kati wa FC Juarez, Julietha Singano inayoshiriki Ligi ya Wanawake Mexico anazidi kung’ara akiingia kwenye kikosi bora cha wiki.
Timu hiyo iko nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi hiyo yenye timu 18, kwenye mechi 14 imeshinda sita, sare nne na kupoteza nne ikikusanya pointi 22.
Nyota huyo ametajwa kwenye kikosi bora cha mzunguko wa 13 Ligi Kuu ya Mexico ikiwa mara yake ya nne kuingia kwenye orodha hiyo.
Singano anakuwa mchezaji pekee kutoka kwenye timu ya Juarez kuingia katika kikosi bora cha michezo ya raundi ya 13 akiwaweka pembeni nyota wa mataifa mbalimbali wanaocheza ligi hiyo.
Huu ni msimu wa tatu mfululizo kwa beki huyo wa timu ya taifa ‘Twiga Stars’ kuichezea timu hiyo akifanikiwa kuingia kwenye kikosi cha kwanza moja kwa moja.
Ndiye beki wa kati tegemeo kwenye kikosi hicho na ndani ya misimu mitatu aliyoitumikia Juarez amecheza jumla ya michezo 73.