Beki JKT Tanzania afichua siri

BEKI wa JKT Tanzania, Wilson Nangu anavutiwa na aina ya ukabaji wa beki wa Simba, Abdulrazak Hamza na Dickson Job wa Yanga.

Nangu amesema jinsi mabeki hao wanaocheza pia Taifa Stars wanavyoonyesha ukomavu wa maamuzi pindi timu wanazozitumikia zikishambuliwa, inamfanya kujifunza mambo mengi sana.

Beki huyo aliyefunga mabao mawili katika Ligi Kuu msimu huu, amesema Hamza na Job wana utulivu unaowasaidia kupiga pasi zinazofika sehemu sahihi, kuokoa hatari bila kusababisha kadi zisizo na ulazima na jicho la kuona hatari za mbali kabla ya kumfikia kipa.

“Siyo kitu kibaya kuwapongeza wanapofanya vizuri na kujifunza baadhi ya mambo kutoka kwao, wanafanya kazi kubwa wakati mwingine mashambulizi unaona kama yanawazidia lakini inashangaza jinsi ambavyo wanaokoa hatari ili timu isifungwe, kitu hicho nimekuwa nikijifunza,” alisema Nangu.

Beki huyo alibainisha kuwa, katika nafasi yake huwa anapambana kuhakikisha haruhusu bao kirahisi huku akipata nafasi ya kufunga anafanya hivyo.

“Ukiona nimefunga ujue nilikuwa katika nafasi hiyo, ila ninachopenda ni kumsaidia kipa apate clean sheet nyingi.”

Nangu alisema matarajio yake kwa mechi zilizosalia kufunga msimu huu kuongeza umakini.

“Zimesalia mechi za hesabu kali ambazo kila mchezaji anapaswa kuongeza umakini katika nafasi yake, mfano kama nafasi yangu lazima niwasome kisawasawa washambuliaji ili nisiwe njia ya kupita kwangu kufunga.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *