Beki Azam atua Ulaya

BEKI wa kushoto raia wa Senegal, Cheick Sidibe amejiunga na klabu ya HJK Helsinki ya Finland akiwa mchezaji huru baada ya kuachana na matajiri wa Chamazi, Azam FC.

Usajili huu unamfanya Sidibe kuwa mchezaji mpya wa kikosi hicho kinachoshiriki Ligi Kuu ya Finland, maarufu kama Veikkausliiga. 

Sidibe amesaini mkataba wa miaka miwili na klabu hiyo, huku kukiwa na kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi kulingana na kiwango chake.

HJK Helsinki, ambayo ni miongoni mwa klabu kubwa Finland, inatarajia mchezaji huyo kuimarisha safu yake ya ulinzi na kuongeza uzoefu wake katika mashindano mbalimbali. 

HJK Helsinki imeonyesha imani kubwa kwa Sidibe na uzoefu wake katika ligi tofauti, ikiwemo Tanzania, utakuwa na manufaa makubwa kwao.

Kocha wa HJK Helsinki, Toni Korkeakunnas kwa upande wake, ameonyesha matumaini beki huyo wa kushoto ataongeza nguvu kwenye kikosi chake kinachojiandaa na msimu mpya wa ligi.

Hata hivyo, kuondoka kwa Sidibe Azam aliyojiunga nayo Julai 2023 akitokea Teungueth FC ya kwao Senegal, hakujaja kwa bahati mbaya. Azam ilionekana kutokuwa na mpango naye kutokana na kiwango bora kinachoonyeshwa na mzawa, Pascal Msindo ambaye ameibuka kuwa chaguo la kwanza katika kikosi cha timu hiyo.

Msindo ambaye amekuwa na msimu mzuri, ameonyesha uwezo mkubwa katika safu ya ulinzi na kushambulia. Katika mchezo wa hivi karibuni wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons, beki huyo alifunga mabao mawili wakishinda 4-0, jambo lililoonyesha mchango wake mkubwa kwa timu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *