
Dar es Salaam. Kama wewe ni mmiliki wa chombo cha moto jua kuwa utatakiwa kuchimba zaidi mfukoni mwako ili kupata mafuta kutokana na bei ya bidhaa hiyo muhimu kupanda huku gharama za uiagizaji zikitajwa kuwa sababu.
Tangu kuanza kwa mwaka huu bei ya rejareja ya petroli, dizeli na mafuta ya taa imeendelea kuongezeka jambo ambalo litaendelea kuathiri uchumi wa watumiaji wa vyombo vya moto.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) leo Machi 5, 2025, bei ya petroli kwa rejareja katika jiji la Dar es Salaam imeongezeka kwa asilimia 6.27, dizeli kwa asilimia 6.73 na mafuta ya taa yakipanda kwa asilimia 12.02.
Kwa mujibu wa taarifa hii iliyosainiwa na Mkurugenzi wake mkuu, Dk James Andilile, ongezeko hilo la bei kwa Machi linafanya petroli sasa kununuliwa kwa Sh2,996 kutoka Sh2,820, dizeli Sh2,885 kutoka Sh2,703 huku mafuta ya taa yakiongezeka zaidi.
Mafuta ya taa sasa yatauzwa Sh3,036 kwa lita moja kwa yale yaliyopitia bandari ya Dar es Salaam kutoka Sh2,710 iliyokuwapo Februari,2025.
Kwa wakazi wa Tanga sasa watanunua petroli rejareja kwa Sh3,042, dizeli kwa Sh2,932 na mafuta ya taa kwa Sh3,082, hiyo ikiwa ni ongezeko kutoka Sh2,825 iliyotumika Februari, 2025 kununua lita moja ya petroli, dizeli kwa Sh2,746 na mafuta ya taa kwa Sh2,756.
Kwa watumiaji wa mafuta yanayopitia bandari ya Mtwara na viunga vyake watanunua mafuta ya petroli lita moja kwa Sh3,069, dizeli kwa Sh2,958 kwa na mafuta ya taa kwa Sh3,108.
Mafuta ya rejareja yaliyopita katika bandari ya Mtwara Februari, 2025 yaliuzwa kwa Sh2,892 kwa lita moja ya petroli, Sh2,775 kwa dizeli na mafuta ya taa kwa Sh2,782.
Hata hivyo, bei ya mafuta kwa Machi inaongezeka wakati ambao gharama za uagizaji mafuta zimeendelea kupungua kwa wastani wa asilimia 0.51 kwa mafuta ya petroli, asilimia 1.91 kwa mafuta ya taa.
Kwa upande wa dizeli gharama za uagizaji zimeongezeka kwa asilimia 24.42 katika Bandari ya Dar es Salaam huku katika Bandari ya Tanga gharama ikipungua kwa wastani wa asilimia 2.60 kwa mafuta ya petroli na dizeli, lakini hakuna mabadiliko katika Bandari ya Mtwara.
Katika tangazo lake la bei mpya Ewura imezitaka kampuni za mafuta kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani isipokuwa isizidi bei kikomo au kuwa chini ya iliyoruhusiwa kama zilivyokokotolewa, kwa mujibu wa Kanuni za Ewura za kupanga Bei za Mafuta za Mwaka 2022.
Pia imevitaka vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei za bidhaa hiyo katika mabango yanayoonekana bayana yakionesha bei za mafuta, punguzo na vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika.
“Wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza mafuta kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani. Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja,” imeeleza taarifa hiyo ya Ewura.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa kutofanya hivyo adhabu itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika, huku wauzaji wa bidhaa za mafuta ya petroli wakitakiwa kutoa stakabadhi za mauzo kutoka kwenye Electronic Fiscal Pump Printers (EFPP). Pia wanunuzi watakiwa kuhakikisha wanapata stakabadhi hizo.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa stakabadhi hizo zinatakiwa kuonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita.
“Stakabadhi hizo zitatumika kama kidhibiti kwa wanunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya kuuziwa kwa bei ya juu kuliko bei kikomo au kuuziwa mafuta yasiyo na kiwango cha ubora unaotakiwa. Pia zitasaidia kurahisisha ukusanyaji wa kodi za Serikali zitokanazo na mauzo ya bidhaa za mafuta ya petroli,” imeeleza taarifa hiyo.