
Geita. Bei ya nyanya katika Soko Kuu la Wakulima Nyankumbu, Manispaa ya Geita, imepanda kwa zaidi ya asilimia 300 kutoka Sh20,000 iliyokuwepo miezi mitatu iliyopita hadi kufikia Sh75,000 kwa tenga.
Kupanda kwa bei hiyo kumeathiri wanunuzi wa rejareja, ambao sasa wanalazimika kununua fungu la nyanya nne kwa Sh1,500, tofauti na Sh500 iliyokuwa awali.
Wafanyabiashara sokoni hapo wanalalamikia hali hiyo, wakidai kuwa ugumu wa kupata nyanya kwa bei nafuu unawafanya kushindwa kuendelea na biashara kwa faida.
Neema Emanuel, mfanyabiashara wa rejareja, akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu, Machi 31, 2025, amesema amekaa sokoni tangu alfajiri bila kupata nyanya za kuuza.
“Niko hapa toka saa 12 asubuhi sijapata nyanya, biashara imekuwa ngumu. Ukifanikiwa kununua, bei haitoi faida. Nyanya ndogondogo zinapatikana kwa Sh60,000, lakini wateja hawazipendi,” amesema Neema.
Kwa upande mwingine, wakulima wa nyanya wamepokea hali hiyo kwa furaha, wakisema kuwa ni wakati wao wa kupata faida baada ya msimu mgumu wa kilimo.
Emanuel Charles, mkulima na muuza nyanya, amesema kupanda kwa bei kumetokana na mabadiliko ya hali ya hewa na mahitaji makubwa kutoka kwa wanunuzi wa nje wanaosafirisha nyanya kwenda Uganda na Rwanda.
“Hali imebadilika ghafla. Juzi tenga lilikuwa linauzwa kati ya Sh8,000 na Sh15,000, lakini sasa linauzwa Sh60,000 hadi Sh80,000. Wanunuzi ni wengi na mavuno ni machache, ndiyo maana bei imepaa,” amesema Emanuel.
Mkulima mwingine, Kevin Damian, amesema kwa sasa ni neema kwa wakulima, kwani hyo ni baada ya kipindi kirefu cha kudharaulika.
“Zamani tulikuwa tunawabembeleza wanunuzi, sasa ni wakati wao wa kutubembeleza sisi! Tenga nauza Sh80,000. Wafanyabiashara wasipokuwa makini na kuuza kulingana na hali ya soko, watajikuta wamekwama na mtaji umekatika,” amesema Damian kwa tabasamu.
Mwenyekiti wa wauza nyanya katika Soko la Nyankumbu, John Malimi, amesema hali inazidi kuwa ngumu kwa wanunuzi wa kawaida, lakini ni neema kwa wakulima.
Amesema ili kukabiliana na changamoto za kupanda na kushuka kwa bei ya bidhaa hiyo, Serikali inapaswa kuingilia kati kwa kujenga kiwanda cha kusindika nyanya ili kudhibiti mabadiliko ya bei yasiyotabirika.
“Kama kungekuwa na kiwanda cha kusindika nyanya, wakulima wangelima kwa uhakika wa soko. Sasa hivi bei inapopanda, ni kilio kwa wafanyabiashara na wateja, lakini neema kwa wakulima,” amesema Malimi.