
Dar es Salaam. Huenda kuongezeka kwa wastani wa gharama za kubadilisha fedha za kigeni kwa asilimia 1.91, Aprili 2025 ikawa sababu ya bei za bidhaa za mafuta kupanda kwa watumiaji wa rejareja nchini.
Kwa sababu, mafuta yanapanda nchini wakati gharama za uagizaji zikipungua kwa viwango tofauti na hata bei yake katika soko la dunia ikishuka.
Ongezeko hili la bei kwa ya petrol, dizeli na mafuta ya taa litaendelea kuathiri uchumi wa watumiaji wa vyombo vya moto kwa kulazimika kutoa fedha zaidi na kupata mafuta kidogo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) leo Aprili 2, 2025, bei kikomo za mafuta kwa Aprili mwaka huu katika soko la dunia zimepungua kwa asilimia 6.92 ya kwa mafuta ya petroli, asilimia 6.57 kwa mafuta ya dizeli na asilimia 7.82 kwa mafuta ya taa.
Bei zinapungua sambamba na gharama za uagizaji mafuta ambapo petroli ilipungua kwa wastani wa asilimia 6.08, asilimia 7.09 kwa mafuta dizeli na imeongezeka kwa asilimia 1.11 kwa mafuta ya taa kwa yanayopitia katika Bandari ya Dar es Salaam.
Katika Bandari Mtwara zimepungua kwa wastani wa asilimia 4.00 kwa mafuta ya petroli na dizeli huku kukiwa hakuna mabadiliko katika bandari ya Tanga.
Taarifa hii iliyosainiwa na Mkurugenzi wake mkuu, Dk James Mwainyekule, sasa wakazi wa Dar es Salaam watanunua lita moja ya petrilo kwa Sh3,037 Aprili mwaka huu kutoka Sh2,996 mwezi uliopita huku dizeli wakinunua kwa Sh2,936 kutoka Sh2,885.
Watumiaji wa mafuta ya taa sasa watanunua lita moja kwa ajili ya matumizi yao nyumbani kwa Sh3,053 kutoka Sh3.036.
Mafuta yanayopitia Bandari ya Tanga ambapo hakukuwa na mabadiliko ya bei ya uagizaji katika soko la dunia wao pia watalazimika kuzama mifukoni zaidi kwani lita moja ya petroli sasa watanunua kwa
Sh3,083 Aprili mwaka huu kutoka Sh3,042, dizeli kwa Sh2,982 kutoka Sh2,932 na mafuta ya taa kwa Sh3,099 kutoka Sh2,958.
Wanunuzi wa mafuta ya rejareja yanayopitia Bandari ya Mtwara na viunga vyake watanunua mafuta ya petroli lita moja kwa Sh3,109, dizeli kwa Sh3,008 na mafuta ya taa kwa Sh3,125.
Ikilinganishwa na mafuta yaliyoingia nchini kupitia Bandari ya Mtwara Machi mwaka huu yaliuzwa kwa Sh3,069 kwa lita moja ya petroli, Sh2,958 kwa dizeli na mafuta ya taa kwa Sh 3,108.
Kufuatia hilo, Ewura imezitaka kampuni za mafuta kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani isipokuwa zisizidi bei kikomo au kuwa chini ya iliyoruhusiwa kama zilivyokokotolewa kwa mujibu wa Kanuni za Ewura za Kupanga Bei za Mafuta za Mwaka 2022.
Pia imevitaka vituo vyote vya mafuta kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayoonekana bayana yakionesha bei za mafuta, punguzo, vivutio vya kibiashara vinavyotolewa na kituo husika.
“Pale ambapo inawezekana kuchagua, wateja wanashauriwa kununua bidhaa za mafuta katika vituo vinavyouza kwa bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani. Ni kosa kuuza mafuta bila kuweka mabango ya bei inayoonekana vizuri kwa wateja,” imeeleza taarifa hiyo ya Ewura iliyosainiwa na Dk Mwainyekule.
Kutofanya hivyo adhabu itatolewa kwa kituo husika kwa kutotekeleza matakwa ya kisheria kwa mujibu wa kanuni husika huku wauzaji wa bidhaa za mafuta ya petroli wakitakiwa kutoa stakabadhi za mauzo kutoka kwenye Electronic Fiscal Pump Printers (EFPP), huku wanunuzi wakitakiwa kuhakikisha wanapata stakabadhi hizo.
Stakabadhi hizo zinatakiwa kuonyesha jina la kituo, tarehe, aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita.
“Stakabadhi hizo zitatumika kama kidhibiti kwa wanunuzi wa mafuta endapo kutajitokeza malalamiko ya kuuziwa mafuta kwa bei ya juu kuliko bei kikomo au kuuziwa mafuta yasiyo na kiwango cha ubora unaotakiwa. Stakabadhi hizo pia zitasaidia kurahisisha ukusanyaji wa kodi za Serikali zitokanazo na mauzo ya bidhaa za mafuta ya petrol,” imeeleza taarifa hiyo.