
Morogoro. Zikiwa zimebaki siku chache kufikia Sikukuu ya Idd, bei ya kuku wa kienyeji imeanza kupanda, huku wafanyabiashara wakidai kuwa upatikanaji wa kitoweo hicho ni mgumu kutokana na hali ya ukame.
Akizungumza na Mwananchi leo, Jumatatu, Machi 24, 2025, mmoja wa wafanyabiashara katika Soko la Kingalu, Shukuru Khasim, amesema wiki mbili zilizopita bei ya kuku ilikuwa kuanzia Sh18,000 hadi Sh25,000, lakini kwa sasa imepanda na kufikia kati ya Sh18,000 na Sh35,000.
Amesema hali ya biashara kwa sasa bado haijawa nzuri, isipokuwa anaamini Sikukuu itakapofika, watafanya biashara nzuri.
Naye Shomari Abdul, mfanyabiashara wa kuku katika Soko la Mawenzi, amesema hali ya ukame katika vijiji wanakotoka kuku kumesababisha upatikanaji wake kuwa mgumu.
“Maeneo tunayochukua kuku ni pamoja na Gairo, Dodoma na Singida. Hata hivyo, kutokana na jua kali, kuku wengi wamekufa kwa magonjwa, hivyo wafugaji nao wamekuwa wakituuzia kwa bei ya juu. Tukileta kuku hapa, inabidi tuuze kwa bei ambayo itatupa faida kidogo,” amesema Abdul.
Wakati huohuo, bei ya nyama katika baadhi ya mabucha ya Manispaa ya Morogoro imeendelea kubaki ile ile ya Sh12,000 kwa kilo moja, ambapo wananchi wameomba wamiliki wa mabucha kutoipandisha hasa kipindi cha sikukuu ya Idd.