Dar es Salaam. Baraza la Wazee la Chadema (Bazecha) limesema licha ya hamahama ya baadhi ya viongozi na wanachama wa chama hicho, uimara wa Chadema sasa ni mkubwa kuliko wakati mwingine wowote.
Baraza hilo limetafsiri hatua ya baadhi ya makada wa chama kujivua nyadhifa zao na kuondoka kama hatua mojawapo inayopitiwa na bahari kutema uchafu.
Chadema inayoendesha kampeni ya “No Reforms No Election” ikilenga kuzuia uchaguzi endapo mabadiliko katika mifumo ya uchaguzi hayatafanyika. Chama hicho kimekuwa kikikosolewa ndani na nje kuhusu ajenda hiyo huku baadhi ya wanachama wake wakiendelea kutangaza kukikacha chama hicho.
Mbali na kampeni hiyo, kupingwa na baadhi ya makada wake, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) inaendelea na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 na hatua inayoendelea sasa ni uboreshaji wa tarifa za wapigakura huku ikiwa imetangaza majimbo mapya.
Katika mkutano wa Baraza hilo na vyombo vya habari, leo Mei 16, 2025 Mwenyekiti wa Bazecha Kanda ya Pwani, James Haule amesema katikati ya hamahama ya wanachama hao chama bado kipo imara.
“Baraza la Wazee baada kufuatilia tumegundua chama kipo imara kuliko wakati mwingine wowote, bahari inatema uchafu, hivyo nitoe wito anayeshuka kwenye basi amefika mwisho wa safari na siasa ina safari ndefu, hao wanaoshuka huenda wasifike nchi ya ahadi wanavyotaka kwenda na kuishia njiani,” amesema.
Hamahama Chadema
Safari ya kukihama chama hicho kwa madai mbalimbali ikiwemo kupinga “No reforms, No Election” (bila mabadiliko hakuna uchaguzi), waliokuwa wajumbe wa sekretarieti ya Chadema walianzisha safari ya kujivua uanachama huku wakieleza kwenda kutafuta jukwaa jingine.
Miongoni mwao ni manaibu katibu mkuu, Benson Kigaila (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar), aliyekuwa mkurugenzi wa itifaki na mambo ya nje, John Mrema, aliyekuwa katibu mkuu wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Catherine Ruge na katibu wa zamani wa sekretarieti, Julius Mwita.
Baada ya kundi hilo kufungua milango, wengine walifuata akiwemo Henry Kilewo, aliyekuwa mwenyekiti wa mkoa wa kichama wa Kinondoni, Patrick Assenga, mhazini wa Kanda Pwani na Emma Kimambo, mhazini Kanda ya Kaskazini.
Wengine ni Gervas Mgonja, mwenyekiti wa Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema, katibu wa Mkoa wa Kilimanjaro na Khadija Mwago, Mwenyekiti wa Bawacha Wilaya ya Mbagala.
Wamo pia Devotha Minja, mwenyekiti wa Kanda ya Kati, Helman Kiloloma, mwenyekiti wa Mkoa wa Temeke, Katibu wa Wilaya ya Segerea, Asha Abubakari, Katibu wa Bawacha Kanda ya Kaskazini, Rachael Sadick na Mwenyekiti wa Bawacha Mkoa wa Kilimanjaro, Grace Kiwelu.

Pia, yumo Esther Fulano, aliyekuwa Katibu wa Bawacha Kanda ya Victoria, Doris Mpatili, Mwenyekiti Kamati ya Mafunzo Kanda ya Victoria, Hanifa Chiwili – Katibu wa Kamati ya Maadili ya Kanda ya Pwani, Mwenyekiti wa Mkoa wa Pwani Kusini na Mussa Katambi na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Kanda ya Magharibi.
Wengine ni Mwenyekiti wa Bawacha Wilaya ya Kilombero, Suzan Kiwanga, Mwenyekiti wa Bavicha Wilaya ya Kilosa, David Chuduo, aliyekuwa mwenyeliti wa Bawacha Wilaya ya Kilosa, Sheila Mluba na mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Tabora, James Kabepele.
Vilevile, Mwenyekiti wa Wilaya ya Kishapu, Boniface Masanja, Katibu wa Bawacha Mkoa wa Shinyanga, Furahisha Wambura, katibu wa jimbo la Msalala, Yussuf Paulo na Hamza Kinyema aliyekuwa Mwenyekiti wa Temeke.
Majeraha Chadema
Kuhusu majeraha ndani ya Chadema baada ya uchaguzi wa ndani, Haule amesema hakuna majeraha yoyote kwa kuwa hakuna malalamiko waliyoyapokea na hata walipowaita wanaodaiwa kuwa na majeraha, hakuna aliyejitokeza.
“Huwezi kusema kuna majeraha kwa sababu hakuna aliyesema ana majeraha, tiba ya kukanyangana kila mtu anatibu majeraha yake,” amesema.
Haule amesema ni jambo la kawaida kutokea mkanyangano wakati wa uchaguzi, hivyo kama yupo aliyekanyagwa anapaswa kutibu majeraha yake.
Amesema baada ya uchaguzi mkuu wa chama hicho, walikaaa na viongozi wote na kuzungumza nao, hivyo hakuna majeraha bali suala la wanachama kuondoka ni demokrasia iliyopo ndani ya chama.
Tiba ya majeraha iliwahi kuzungumziwa pia na Mwenyekiti mstaafu Freeman Mbowe baada ya uchaguzi wa chama hicho kukamilika, akiwataka viongozi wapya kutibu majeraha ya uchaguzi ndani ya chama hicho.
Wanaunga mkono No Reforms
Katika hatua nyingine, Haule amesema kazi inayofanywa na viongozi wakuu wa chama hicho ya kuendelea na kampeni ya kudai mageuzi kabla ya uchaguzi, wanaunga mkono na wapo nyuma yao kwa kila hatua.
Amesema viongozi wao wanapitia changamoto ya kukandamizwa, hivyo ni muhimu Rais Samia Suluhu Hassan kuelekeza vyombo vya ulinzi kuacha tabia hiyo na badala yake demokrasia itawale.
“Tunatoa wito kwa Rais Samia kutoka hadharani kwa kuwa yeye ndio mfariji wa nchi kwanini Watanzania wananyanyasika kwenye ardhi yao na hatua gani amechukua,” amesema.
Pia, baraza hilo limewahimiza Watanzania kujitokeza Mei 19, 2025 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusikiliza kesi ya mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu pamoja na kumpa pole.
Tayari mawakili wa Lissu, Jebra Kambole na Peter Kibatala wametoa maelekezo kwa wote watakaofika mahakamani hapo wahakikishe wanakuwa watulivu.