Usiku wa Ulaya umeendelea kuwa na maajabu yake hasa pale timu inayopewa nafasi ya kufanya vizuri ishindwe kutamba na hicho ndicho kimezikuta AC Milan na Atalanta kwenye hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya jana usiku.
AC Milan imeaga mashindano hayo baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani dhidi ya Feyenoord ambayo ilikuwa na faida ya ushindi wa bao 1-0 nyumbani hivyo ikasonga katika hatua ya 16 bora kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1.

Club Brugge wakishangilia baada ya kuichapa Atalanta 3-1 ugenini na kusonga mbele katika hatua ya 16 bora.
Atalanta iliyopewa nafasi kubwa ya kupindua meza dhidi ya Club Brugge ambayo mechi ya kwanza ilishinda mabao 2-1 ilijikuta katika wakati mgumu katika kipindi cha kwanza kwani ilienda mapumziko ikiwa imefungwa mabao 3-0.
Mabao ya Brugge yalifungwa na Chemsdine Talbi ambaye alipachika mawili katika dakika ya tatu na dakika ya 27 huku lingine likifungwa na Ferran Jutgla.
Bao pekee la kufutia machozi la Atalanta lilifungwa na Ademola Lookman katika dakika ya 46.
Baada ya ushindi huo dhidi ya Atalanta, Club Brugge inafuzu katika hatua ya 16 bora kwa jumla ya mabao 5-2.

Kuondolewa kwa AC Milan na Atalanta kunaifanya Italia kubakiza wawakilishi wawili katika Ligi ya Mabingwa Ulaya ambazo ni Inter Milan iliyofuzu katika hatua ya 16 bora na Juventus ambayo ipo kwenye mchujo.
Nchini Ujerumani kwenye Uwanja wa Alianz Arena ilisubiriwa hadi dakika za mwisho kuiona Bayern Munich ikifuzu katika hatua ya 16 bora baada ya Alphonso Davies kusawazisha bao dakika za lała salama dhidi ya Celtic ambayo bao lake lilifungwa dakika ya 63 na Nicolas Kuhn.

Bayern imefuzu katika hatua ya 16 bora kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-2 baada ya mchezo wa kwanza uliochezwa Scotland kuifunga Celtic kwa mabao 2-1.
Mchezo mwingine ulichezwa Ureno ambapo Benfica ilifanikiwa kwenda katika hatua ya 16 bora baada ya kupata sare ya mabao 3-3 dhidi ya AS Monaco.

Sare hiyo iliibeba Benfica kupata ushindi wa jumla wa mabao 4-3 kwani katika mchezo wa kwanza ilipata ushindi wa bao 1-0 ilipokuwa Ufaransa.
Hatua nyingine ya mtoano katika Ligi ya Mabingwa Ulaya itaendelea tena leo kwenye viwanja vinne tofauti ambapo timu nne zitafuzu katika hatua ya 16 bora.
Mechi za leo Ligi ya Mabingwa Ulaya
Real Madrid vs Manchester City
Borussia Dortmund vs Sporting CP
PSV Eindhoven vs Juventus
PSG vs Brest