Bayern yagomea ofa ya Man United

Munich, Ujerumani. Ofa mbili zilizopelekwa na Manchester United jana jioni kwa ajili ya kumtaka staa wa Bayern Munich Mathys Tel, zimegomewa.

Awali ilielezwa kuwa United ipo tayari kumsajili kinda huyo, lakini timu hiyo ambayo jana ilipoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Crystal Palace imeshindwa kutimiza masharti ya mkopo.

Hii inakuwa timu ya pili kutoka England kushindwa kumsajili mchezaji huyo mwenye miaka 19 baada ya awali Bayern kugomea ofa ya Tottenham.

Baada ya dili la mshambuliaji huyo kushindikana sasa United imehamishia nguvu kwa staa wa Chelsea Christopher Nkunku, ingawa bado kunaonekana kuwa na ugumu wa kumpata.

United, ambayo imeshamruhusu mshambuliaji wa Marcus Rashford kujiunga na Aston Villa kwa mkopo, bado pia inaaminika inaweza kupata saini ya Leon Bailey kutoka Aston Villa kwa mkopo hadi mwishoni mwa msimu.

Tel amekuwa mmoja kati ya wachezaji wanaowaniwa na timu nyingi za Ligi Kuu England kwenye dirisha hili la Januari lakini timu zote zimeshindwa kufikia dau lake la pauni 50 milioni linalotakiwa na Bayern ambayo haimtumii kwenye michezo mingi.

Kocha wa United, Ruben Amorim anatakiwa kuhakikisha anafanya usajili wa mshambuliaji mmoja kabla dirisha halijafungwa leo usiku kwa kuwa anaonekana hana imani na Joshua Zirkzee pamoja na Rasmus Hojlund.

Mastaa hao wawili walianzia kwenye benchi kwenye mchezo wa Ligi Kuu England jana dhidi ya Crystal Palace ambao United ililala kwa mabao 2-0 na aliamua kumuanzisha Kobbie Mainoo ambaye siyo mshambuliaji rasm

Kama Tel ambaye ameshafunga mabao 16 kwenye mechi  83 za Bundesliga ambazo ameichezea Bayern atajiunga na United anaweza kupunguza uhaba wa mabao kwenye kikosi hicho msimu huu.

Hadi sasa United ambayo ipo nafasi ya 13 imekusanya pointi 29, imefunga mabao 28 tu lakini safu yake ya ulinzi imeruhusu mabao 34 kwenye michezo 24 iliyocheza.