
Dodoma. Wizara ya Kilimo imewasilisha bungeni bajeti ya Sh1.243 trilioni kwa mwaka wa fedha wa 2025/26, inayolenga kuendeleza miradi iliyopo na kuanzisha mipya, ili kuimarisha uhimilivu katika sekta hiyo.
Bajeti iliyopendekezwa ni pungufu kwa Sh5 bilioni, ikilinganishwa na Sh1.248 trilioni iliyopitishwa na Bunge katika mwaka wa fedha wa 2024/25.
Miradi ya maendeleo imetengewa Sh1.011 trilioni, ikilinganishwa na Sh1.033 trilioni mwaka 2024/25, huku matumizi ya kawaida yakipata ongezeko la Sh15.4 bilioni na kufikia Sh231.28 bilioni.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amewasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake leo Jumatano, Mei 21, 2025 bungeni jijini Dodoma. Wabunge wataijadili kwa siku mbili Mei 21 na 22, 2025.
Bashe amesema katika mwaka 2025/26, wizara itaendeleza vipaumbele vya kimkakati sita na kuongeza idadi ya mipango mkakati kutoka 27 hadi 31.
Bashe ameyataja maeneo muhimu ni pamoja na kuongeza thamani ya bidhaa, kuimarisha utafiti, maendeleo ya umwagiliaji, matumizi ya zana bora, ushirikishwaji wa kifedha, na usalama wa chakula.
Amesema wizara imepanga kujenga kiwanda cha vifaa vya matibabu kikitumia pamba inayozalishwa nchini, kuanzisha kongani ya viwanda vya pamba mkoani Simiyu na kujenga kituo cha utafiti wa baiolojia na benki ya vinasaba.
“Hatua hiyo itaipunguzia nchi gharama za kuagiza pamba za hospitali na nyuzi kwa ajili ya zao la tumbaku; na kupunguza gharama ya uagizaji wa vifaa tiba vinavyotokana na pamba kwa Dola za Marekani 17 milioni na vifungushio vya tumbaku,” amesema.
“Tunakusudia kujenga maabara za kuzalisha miche kwa njia ya chupa kwa kila kituo cha Utafiti wa Kilimo (Tari) na ujenzi wa vituo 1,000 vya kutoa huduma ya zana za kilimo kwa wakulima kwa mfumo wa ruzuku,” ameongeza.
Amesema bajeti hiyo pia inapendekeza kupanua miundombinu ya umwagiliaji katika bonde la Bugwema, Ngono na Rufiji, na kutekeleza mradi wa usambazaji maji kutoka Ziwa Victoria na Tanganyika ili kufaidisha mikoa 12, wilaya 69, kata 192 na vijiji 943.
Amesema pia bajeti hiyo itaweka mkazo katika ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani kupitia ushirika, kiwanda cha kusindika tumbaku mkoani Tabora, kongani ya viwanda vya kubangua korosho mkoani Mtwara na ununuzi wa ndege ili kuimarisha kilimo anga nchini.
Wizara pia ina mpango wa kuanzisha mfuko wa hisa na dhamana katika Benki ya Ushirika ya Tanzania na kwamba mazungumzo yanaendelea baina ya wizara hiyo na Wizara ya Fedha ili kuanzisha mfumo wa kodi utakaolinda bidhaa za kilimo za ndani, hasa mafuta ya kula na ngano.
Amesema malengo ya uzalishaji wa kimkakati ni pamoja na kuongeza uzalishaji wa mazao muhimu kutoka tani milioni 1.45 hadi tani milioni 2.22, kuongeza mazao ya chakula kutoka tani milioni 22 hadi tani milioni 23, na kuongeza kujitosheleza kwa kwa chakula hadi asilimia 130.
“Malengo mengine ni kuongeza thamani ya uuzaji nje wa bidhaa za kilimo kutoka Dola za Marekani 3.54 bilioni (Sh9.5 trilioni) hadi Dola za Marekani 4 bilioni (Sh10.7 trilioni) na kupanua hekta za umwagiliaji hadi milioni 1.2.
Utafiti, upatikanaji wa mbegu bora
Bashe ameliambia Bunge wizara yake itaendelea kuwekeza katika utafiti wa mbegu, pamoja na kujenga kituo cha baiolojia Tari Ilonga na benki ya mbegu huko Tari Selian.
Amesema wizara pia inapanga kumalizia ujenzi wa maabara ya utengenezaji wa miche kwa njia ya chupa na kufanya utafiti juu ya aina 56 za mbegu.
Kwa mujibu wa waziri huyo, wizara yake inakusudia kuzalisha tani 655.24 za mbegu za msingi za mazao ya kimkakati na kuhifadhi aina 360 za mbegu asilia.
“Hekta 2,121 za miundombinu ya umwagiliaji zitajengwa katika mashamba ya utafiti,” amesema.
Miundombinu ya umwagiliaji
Kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Bashe amesema Wizara ya Kilimo itatekeleza miradi 768, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mabwawa huko Mbakiamtuli na Ngorongo katika Bonde la Rufiji, yenye uwezo wa mita za ujazo milioni 57 kwa ajili ya kumwagilia hekta 64,800.
Amesema miradi 114 ipo katika hatua ya upembuzi yakinifu na ujenzi wa mabwawa yenye takriban mita za ujazo bilioni 1.18 ambapo kati ya hayo, mabwawa 19 yyapo hatua ya ujenzi na mawili yamekamilika.
“Aidha, mabwawa 28 yametangazwa kwa ajili ya ujenzi na 65 usanifu unaendelea,” amesema.
Amesema miundombinu ya umwagiliaji inakusudiwa kujengwa katika mabonde ya Mto ya Ngono na Bugwema kwa ajili ya kumwagilia hekta 22,770.
“Zabuni ya kumpata mshauri elekezi kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu wa kutumia maji ya Ziwa Victoria na Tanganyika kwa ajili ya shughuli za kilimo imetangazwa,” amesema.
“Ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji katika skimu 101 zenye jumla ya hekta 219,608.46 na ujenzi wa mabwawa 47 yenye mita za ujazo milioni 813.8 ni miongoni mwa miradi itakayotekelezwa na Wizara mwaka ujao wa fedha,” aliongeza.
Waziri Bashe amesema mipango iko katika hatua za awali ya kubuni miradi minane ya mabonde na kuandaa miradi 65 ya mabwawa mapya.
Ameliambia Bunge kuwa wizara itaunda mfumo wa usimamizi wa ardhi kwa mashamba ya Membe, Bugwema, Madibira, na Lumpungu na kununua shamba la Mbarali lenye ukubwa wa hekta 2,575, litakalotolewa kwa wakulima wadogo.
Amesema Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) itajenga mabwawa ya Dudumizi na Mambi katika shamba hilo.
Zana bora za kilimo
Ili kuimarisha matumizi ya zana bora za kilimo, Bashe amesema wizara imepanga kuanzisha vituo 1,000 vya huduma na kununua matrekta 10,000 na zana zote za msingi zinazohitajika kwa ajili ya kufanya kazi za shambani, power tiller 10,000, mashine za kuvuna, kukaushia pamoja na vifaa vyote muhimu vya zana za kilimo.
“Wizara imepanga pia kuanzisha kituo kimoja cha kitaifa (national mechanization centre) ambacho kitakuwa na zana zote za msingi kwa ajili ya kusafisha na kusawazisha mashamba, uchimbaji wa visima na mabwawa na kutoa mafunzo,” amesema.
“Wizara itatoa mafunzo kuhusu uendeshaji na usimamizi wa zana za kilimo kwa waendesha mitambo, wasimamizi wa vituo na watoa huduma 500 kwa kushirikiana na Camartec na Veta,” ameongeza.
Uzalishaji mazao asilia ya biashara
Bashe amesema Serikali imeweka mikakati ya kuongeza uzalishaji wa mazao asilia ya biashara na kubainisha kuwa uzalishaji wa pamba unatarajiwa kuongezeka kutoka tani 149,361 hadi tani 400,000, kahawa kutoka tani 81,366 hadi tani 85,000 na korosho kutoka tani 528,264 hadi tani 700,000.
“Uzalishaji wa tumbaku unatarajiwa kuongezeka kutoka tani 160,000 hadi tani 200,000. Wizara pia itawasajili wakulima 91,000 wa kakao na kusambaza miche milioni moja ya zao hilo katika mikoa ya Tanga, Kigoma, Kagera na Morogoro,” amesema.
“Mauzo ya parachichi nje yanatarajiwa kuongezeka kutoka tani 35,627 hadi tani 40,000 kupitia usambazaji wa miche milioni 2.1, wakati uzalishaji wa ngano unatarajiwa kukua kutoka tani 118,521 hadi tani 300,000,” aliongeza.
Ametoa rai kwa wasindikaji wa ngano nchini, kuiunga mkono Serikali katika juhudi zake kwa kununua ngano inayozalishwa nchini kabla ya kuagiza kutoka nje, kama ilivyokubaliwa kwenye mikataba yao na Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA).
Amesema Serikali itaanza kufanya tathmini kwa wawekezaji waliobinafsishiwa viwanda vya kusindika chai na kushindwa kuviendesha ili kuona namna ya kuvirejesha kwa wakulima kwa kuzingatia sheria zilizopo.
Sukari na mafuta ya kula
Kwa mujibu wa Bashe, Tanzania inakusudia kuzalisha tani milioni 7.2 za miwa itakayozalisha tani 700,000 za sukari.
Amesema ingawa nchi bado inaagiza tani 150,000 za sukari ya viwandani kila mwaka, uzalishaji wa sukari ya kawaida unaendelea kuwa bora.
“Serikali inakusudia kubadili mfumo wa uingizaji wa sukari ya viwandani na haki ya uingizaji wa sukari ya viwandani ambapo kuanzia mwaka ujao itakuwa chini ya viwanda vinavyozalisha sukari ndani ya nchi,” alisema.
Kuhusu mafuta ya kula, Bashe alisema uzalishaji kwa sasa ni tani 396,335 ikilinganishwa na mahitaji ya tani 650,000—hivyo kuacha pengo la tani 253,665.
Ili kukabili upungufu huu, alisema wizara imepanga kuzalisha tani 2,150 za mbegu bora za alizeti, chini ya mpango wa ruzuku na kusambaza miche milioni 10 ya michikichi kwa wakulima.
Amesema pia msaada utatolewa kwa wakulima wadogo katika sekta za alizeti na michikichi.
“Serikali itaendelea kushirikiana na Wizara ya Fedha kufanya mageuzi ya sera za kodi, ikiwa ni pamoja na kuongeza ushuru wa uagizaji ngano na mafuta ya kula, ili kulinda wazalishaji wa ndani,” alibainisha.
Amesema wizara yake itaanza majadiliano na Wizara ya Nishati kuweka ruzuku ya umeme kwenye kongani za viwanda vya mafuta ya kula katika mikoa ya Singida na Kigoma ili kuwapa nafuu wawekezaji.
Uwezeshaji vijana na wanawake (BBT)
Waziri Bashe amesema Mfuko wa Pembejeo (AGITF) kwa kushirikiana na Benki ya Ushirika Tanzania, utaanzisha dirisha maalumu litakalotoa huduma za dhamana kwa mikopo yenye riba nafuu na fedha za awali zitakazowekezwa ni kutoka Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kiasi cha Dola za Marekani 35 milioni.
“Pia, Wizara kupitia AGITF itaweka Sh 17 bilioni katika dirisha la dhamana ili kutoa mikopo yenye riba nafuu ya thamani ya Sh51 bilioni kwa wakulima kwa riba isiyozidi asilimia saba,” amesema.
Amebainisha kuwa wizara itaanza majadiliano na Wizara ya Fedha kwa ajili ya kufungua akaunti ya Serikali kwenye Benki ya Ushirika Tanzania.
Katika mradi wa Kujenga Kesho iliyo Bora (BBT), Bashe alisema Wizara ya Kilimo itaanzisha shamba la Mapogolo lenye ekari 20,000 wilayani Chunya, mkoani Mbeya, litakalojumuisha makazi, miundombinu ya umwagiliaji na maghala.
Amebainisha mpango wa wizara yake wa kujenga maghala manane katika mashamba ya vijana ya Chinangali na Mlazo/Ndogowe jijini Dodoma, kujenga uzio wa umeme wa kilomita 27 na chumba cha baridi (cold room) chenye uwezo wa kuhifadhi tani 1,000.
Amesema Serikali za mitaa pia zitasaidia umwagiliaji kwa wakulima wadogo, upatikanaji wa fedha kwa vijana na wanawake, na utekelezaji wa miradi ya BBT.
Usalama na uhifadhi wa chakula
Kwa mujibu wa Bashe, Serikali inakusudia kuongeza uwezo wa kuhifadhi chakula kufikia tani milioni tatu ifikapo 2030.
“Hii itahusisha kukamilisha miradi ya hifadhi tani 165,000 na kujenga uwezo wa ziada wa tani 300,000 katika maeneo ya Songea, Makambako, Songwe, Shinyanga na Dodoma,” amesema.
“Tutaimarisha pia uwezo wa Wakala wa Hifadhi ya Chakula ya Taifa (NFRA) kununua moja kwa moja mazao kutoka kwa wakulima na kuhamasisha matumizi ya vyakula vyenye virutubisho kupambana na utapiamlo nchini,” amesema.
Masoko na matumizi ya Tehama
Waziri huyo amesema bajeti ya Wizara ya Kilimo inakusudia kuboresha miundombinu na upatikanaji wa masoko ya ndani na nje ya nchi.
Amesema msisitizo utawekwa katika kuongeza thamani, ushirikiano na sekta binafsi, kuboresha upatikanaji wa fedha, na kuhakikisha viwango vya ubora vinakidhi matakwa ya soko la kimataifa.
Amesema wizara yake imepanga kukuza maendeleo ya ushirika na kupanua matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) katika mnyororo wa thamani wa kilimo.