Bashe: Ni miaka minne ya mapinduzi kwenye kilimo

Bashe: Ni miaka minne ya mapinduzi kwenye kilimo

Dodoma. Wizara ya Kilimo imetaja mafanikio yaliyopatikana katika sekta hiyo kwa kipindi cha miaka minne iliyopita, yakichangiwa na uwekezaji wa umma, upatikanaji wa pembejeo, huduma bora za utafiti na ugani, pamoja na ongezeko la uzalishaji.

Akiwasilisha bajeti ya Sh1.243 trilioni kwa mwaka wa fedha wa 2025/26 bungeni jijini Dodoma leo Jumatano, Mei 21, 2025, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amebainisha mikakati ya kimuundo kuanzia upanuzi wa umwagiliaji na mifumo ya ushirika, kupunguza utegemezi wa bidhaa toka nje na kuongeza mauzo ya bidhaa za kilimo nje ya nchi yamechangia mafanikio hayo.

Amesema Serikali ya awamu ya sita, iliyoingia madarakani Machi 2021, ilirithi changamoto kadhaa ikiwemo ufinyu wa bajeti, uhaba wa mikopo, ukosefu wa fedha maalumu za kuendeleza kilimo, pamoja ushiriki mdogo wa vijana na wanawake kutokana na ukosefu wa mtaji na umiliki wa ardhi.

“Miundombinu ya kuhifadhi bidhaa za kilimo iliendelea kuwa hafifu, ushirika ulikuwa dhaifu na masoko hayakuwa na ushindani. Tuliendelea kuagiza ngano, sukari na mafuta ya kula kwa sababu ya uzalishaji mdogo ndani ya nchi,” amesema.

Ametaja changamoto nyingine za bei zisizo za uhakika za pembejeo, athari zilizoongezeka kufuatia mlipuko wa janga la Uviko-19, ucheleweshaji katika Bandari ya Dar es Salaam, upungufu wa huduma za ugani na vifaa, uwezo duni wa kudhibiti wadudu na magonjwa, uzalishaji mdogo wa mbolea na upungufu wa wataalamu wa umwagiliaji.

“Changamoto hizi ziliathiri sana watu wetu hivyo kuendelea kubaki kwenye umasikini na kuifanya sekta ya kilimo isivutie na isiwe rasmi. Ziliathiri pia ukuaji wa sekta, mauzo ya mazao ya kilimo nje ya nchi, kiwango cha usalama wa chakula, upatikanaji wa mitaji na pembejeo, tija na uzalishaji wa mazao,” amesema.

“Maeneo mengine yaliyoathirika ni pamoja na mtandao wa miundombinu ya umwagiliaji na uwekezaji mdogo katika uzalishaji wa mbegu bora,” ameongeza.

Amesema ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 ililenga kuimarisha ushirika wa hiari wa wananchi chini ya usimamizi wa Serikali, kuboresha umwagiliaji, kuongeza huduma za utafiti na ugani, kuboresha upatikanaji wa masoko, na kutoa ajira kwa vijana.

Rais Samia Suluhu Hassan alikazia vipaumbele hivi katika hotuba yake ya ufunguzi Bunge mnamo Aprili 2021 na kutaka hatua za haraka zichukuliwe ili kuongeza uzalishaji wa mazao kupitia tafiti, uzalishaji wa mbegu, upanuzi wa umwagiliaji na upatikanaji wa pembejeo bora za kilimo.

Bajeti na maendeleo ya sekta

Waziri Bashe aliliambia Bunge kuwa katika kukabiliana na changamoto hizo, kufikia Aprili 2025, bajeti ya Wizara hiyo imeongeza kwa asilimia 324.5—kutoka Sh294 bilioni mwaka wa fedha 2021/22 hadi Sh1.248 trilioni mwaka 2024/25.

Amesema ukuaji wa sekta umeimarika—kutoka asilimia 2.6 mwaka 2021 hadi asilimia 4.2 mwaka 2023, na makadirio ni kukua kwa ya asilimia tano 2025 na asilimia 10 ifikapo 2030.

“Thamani ya mauzo ya mazao ya kilimo nje ya nchi iliongezeka kutoka Dola za Marekani 1.2 bilioni mwaka 2019/20 hadi Dola za Marekani 3.54 bilioni mwaka 2023/24—ongezeko la asilimia 195,” amesema.

Uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kwa asilimia 33 kutoka tani milioni 17.14 mwaka 2021/22 hadi tani milioni 22.8 mwaka 2023/24 na kufikia asilimia 128 ya kujitosheleza kwa chakula—karibu na lengo la asilimia 130 kitaifa.

Uzalishaji wa mahindi umeongezeka kwa asilimia 91 hadi tani milioni 12.26, na kufanya Tanzania kuwa mzalishaji mkubwa wa pili wa mahindi Afrika, wakati uzalishaji wa mchele umeongezeka kwa asilimia 72 hadi tani milioni 3.04 katika kipindi hicho.

Uzalishaji wa mazao ya biashara

Bashe amesema uzalishaji wa mazao ya biashara umeongezeka kwa asilimia 61.5 kutoka tani 898,967 mwaka 2020/21 hadi tani 1.45 milioni mwaka 2023/24.

Amesema uzalishaji wa korosho umeongezeka kwa asilimia 151 hadi tani 528,263, na uzalishaji wa tumbaku uliongezeka kwa asilimia 173 hadi tani 160,000, na kufanya Tanzania kuwa mzalishaji mkubwa wa pili Afrika.

“Uzalishaji wa miwa umeongezeka kwa asilimia 17 hadi tani milioni 4.71, na kuzalisha tani 431,736 za sukari—asilimia 81.7 ya mahitaji ya kitaifa,” alisema.

Aidha, amesema uzalishaji wa mkonge umeongezeka kwa asilimia 69, huku uzalishaji wa kahawa ukiongezeka kwa asilimia 37 hadi tani 81,366, na kufanya Tanzania kushika nafasi ya nne Afrika.

Amesema upatikanaji na usambazaji wa mbegu bora umefikia tani 79,700 sawa na asilimia 99.6 ya lengo la kuzalisha na kuthibitisha tani 80,000 za mbegu dhidi ya mahitaji ya tani 127,650.

“Kati ya hizo, tani 63,526 zimezalishwa ndani ya nchi na tani 16,174 zimeingizwa kutoka nje ya nchi,” alisema na kuongeza.

“Tani 700 za mbegu bora za alizeti na tani 500 za mbegu bora za ngano zenye thamani ya Sh17.38 bilioni zimesambazwa kwa wakulima katika maeneo ya uzalishaji kupitia mpango wa ruzuku.”

Amesema uzalishaji wa mbegu za mafuta umeongezeka kwa asilimia 25 hadi tani milioni 2.14, na uzalishaji wa alizeti umeongezeka kwa asilimia 154 hadi tani milioni 1.21.

Uzalishaji, matumizi ya mbolea

Amesema uzalishaji wa mbolea nchini umeongezeka kwa asilimia 392 – kutoka tani 32,239 hadi tani 158,628 – ukichagizwa na ufunguzi wa kiwanda kipya jijini Dodoma na upanuzi katika kiwanda cha Minjingu.

Vilevile, upatikanaji wa mbolea umeongezeka kwa asilimia 79 hadi tani 1.21 milioni, ambapo tani 1.45 milioni zenye thamani ya Sh708.62 bilioni zilisambazwa kwa wakulima katika mpango ruzuku.

Matumizi ya mbolea, nayo yameongezeka kwa asilimia 133 hadi tani 848,884, wakati matumizi ya wastani kwa hekta yameongezeka kutoka kilogramu 19 hadi kilogramu 24, sawa na asilimia 48 ya lengo la Programu ya Maendeleo ya Kilimo ya Afrika (CAADP) la kilogramu 50 kwa hekta.

Hifadhi ya chakula na umwagiliaji

Waziri Bashe alisema uwezo wa hifadhi ya chakula kitaifa umeongezeka kwa zaidi ya asilimia 209, kutoka tani 251,000 mwaka 2020/21 hadi tani 776,000 mwaka 2024/25.

Idadi ya miradi ya umwagiliaji imeongezeka kutoka 13 mwaka 2020/21 hadi 780 mwaka 2024/25, yenye thamani ya Sh1.34 trilioni ikihudumia hekta 543,366.

Alisema ukamilishaji wa miradi hii utaongeza eneo la umwagiliaji hadi hekta 1.27 milioni, na kwamba miradi ya ushirika imeongezeka kutoka 19 hadi 912.

Utafiti, ugani na zana za kilimo

Amesema Wizara imekamilisha ujenzi wa Kituo cha udhibiti wa visumbufu vya mimea kibailojia – Kibaha, na maabara ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania – Dar es Salaam.

Bashe alisema Wizara pia imepata ithibati ya kimataifa kwa maabara ya udongo na mimea ya Tea Research Institute of Tanzania (TRIT).

“Kwa kuboresha huduma za ugani, wizara iligawa magari 44, pikipiki 6,444, vifaa vya afya ya udongo 143, kompyuta kibao 5,426, na vifaa vya kazi 1,662, na kujenga nyumba 50 kwa maafisa ugani,” alisema.

Kwa upande wa mitambo, alisema trekta 500 na mashine za kilimo 800 zilinunuliwa, na kiwanda cha usindikaji zabibu chenye uwezo wa kuchakata tani 300 kwa mwaka kimekamilika Dodoma, pamoja na kituo cha usimamizi wa mavuno Mtanana.

Uzalishaji ajira na pembejeo

Mradi wa maendeleo ya kilimo ilizalisha zaidi ya ajira milioni moja za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, katika maeneo ya utafiti, ujenzi, ukarabati na usanifu wa miradi ya umwagiliaji, programu ya Jenga Keshome.

Pia amesema miongoni mwa mafanikio ni kuanzishwa Benki ya Ushirika ya Tanzania kwa mtaji wa Sh58 bilioni na tayari imefungua matawi manne – Dodoma, Kilimanjaro, Tabora na Mtwara na kwamba imesajili vyama vikuu vya ushirika 58 kuwa mawakala wa benki hiyo.

“Serikali imeimarisha matumizi ya mizani ya kidijiti kwenye ununuzi wa mazao ya wakulima ambapo jumla ya mizani 3,760 yenye thamani ya Sh13.3 bilioni imenunuliwa na kusambazwa kwa vyama vya ushirika 992,” alisema.

“Imeongeza ajira katika vyama vya ushirika kutoka 100,100 mwaka 2020/2021 hadi 155,106 mwaka 2024/2025 sawa na ongezeko la asilimia 55.1,” aliongeza.

Bashe alisema serikali imeongeza viwanda vinavyomilikiwa na vyama vya ushirika kutoka 267 mwaka 2021/2022 hadi 331 mwaka 2024/2025 vikijihusisha na uchambuaji wa pamba; ukoboaji wa mpunga, kahawa na mahindi.

Vyama vingine, alisema vinajihusisha na usindikaji wa maziwa; ukamuaji wa mafuta ya pamba, alizeti, karanga na ufuta; na ubanguaji wa korosho.

“Akiba katika vyama vya akiba na mikopo (Saccos) imeongezeka kutoka Sh576 bilioni hadi Sh966.9 bilioni, wakati mikopo iliyotolewa kwa wanachama imeongezeka kutoka Sh798 bilioni hadi Sh1.1 trilioni na ripoti za ukaguzi safi zimeongezeka kutoka 339 hadi 631,” aliongeza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *