Bashe atangaza mabadiliko mfumo wa malipo wakulima wa korosho

Tunduru. Serikali ya Tanzania imetangaza kuwa wakulima wa korosho watalipwa moja kwa moja na vyama vya ushirika, badala ya Vyama vya Ushirika vya Msingi (Amcos) kuanzia msimu wa 2024/25.

Mabadiliko hayo makubwa katika mfumo wa malipo yanakusudia kumaliza changamoto zinazowakabili wakulima wakati wa msimu wa mauzo ya korosho ikiwemo kucheleweshwa malipo na kupoteza mapato.

Malipo yatafanyika kupitia mfumo mpya uitwao Central Payment System ambao umepata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa majaribio yaliyofanywa kwenye  chama cha ushirika cha Lindi Mwambao, mwaka jana.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, alitangaza mabadiliko hayo wilayani Tunduru, Mkoa wa Ruvuma, jana Jumamosi, Septemba 21, 2024, wakati wa ziara yake ya kikazi inayoendelea kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa chini yake.

Wakati wa ziara hiyo, Bashe alifanya mazungumzo na wabunge na madiwani wa Tunduru kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu wananchi hususan wakulima.

“Kwa mfumo huu, vyama vya ushirika vitakuwa vinawalipa wakulima wa korosho mojamoja baada ya makato yote muhimu kufanyika,” aliwaambia wabunge na madiwani.

Awali, miongozo iliwataka wanunuzi kuweka fedha kwenye vyama vya ushirika saa kadhaa baada ya mnada, kutumwa kwenye Amcos kwa ajili ya kuwalipa wakulima baada ya makato muhimu kufanyika.

Hata hivyo, katika mfumo huu mpya wakulima watapokea malipo yao moja kwa moja kutoka vyama vya ushirika na kuziweka kando Amcos ambazo zilitumika kufanya malipo hayo katika mfumo wa zamani.

“Upinzani utawepo kwa sababu watu hawajazoea mabadiliko. Pili, inawezekana wapo viongozi wa Amcos waliokuwa wanatumia mfumo wa zamani kujinufaisha, hivyo hawawezi kufurahia mabadiliko haya,” alisema Waziri Bashe.”

“Wananchi wasiwe na wasiwasi, kupitishwa kwa mfumo mpya mara nyingi kunaambatana na changamoto kadhaa kabla ya kuleta matokeo yaliyotarajiwa,” alisema, akirejea changamoto za awali wakati wa uanzishaji wa mfumo wa utoaji wa mbolea za ruzuku.

Bashe alisema Serikali inafikiria kupanua mfumo huo wa malipo kwenye mazao mengine ili kushughulikia changamoto za malipo kwa wakulima nchini.

Uanzishaji wa mfumo huo ulichochea tofauti ya mtazamo miongoni mwa wabunge na madiwani wa Tunduru, huku baadhi wakiunga mkono na wengine kupinga.

Walichokisema wabunge

Mbunge wa Tunduru Kusini (CCM), Daimu Mpakate, alisema ana wasiwasi kuhusu hujuma, akashauri kwamba utekelezaji unaweza kuanza na mazao madogo ya kilimo kama ufuta.

“Ingawa mfumo ni mzuri, utekelezaji wake unafanywa katika wakati usio sahihi,” alisema.

Mbunge wa Tunduru Kaskazini (CCM), Hassan Kungu, aliunga mkono utambulisho wa mfumo huo akisema unalenga kutatua kilio cha malipo ya wakulima.

“Malipo ya wakulima wa korosho yamekuwa na matatizo kwa miaka mingi. Mkuu wa Wilaya wa zamani, Julius Mtatiro, aliwahi kuwakamata na kuwaweka rumande baadhi ya viongozi wa Amcos kwa kutumia vibaya mfumo wa malipo ya wakulima wa korosho,” alisema.

Mitazamo ya viongozi

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru, Hairu Mussa alisema mlolongo wa ufujaji fedha ni mrefu, ukianzia kwenye vyama vya ushirika.

“Kwa upande wangu, ninaunga mkono uamuzi huo kwa sababu hali ni mbaya katika wilaya hii. Mtu anaandikisha idadi ya mikorosho katika shamba lake, lakini nambari ya simu iliyoandikishwa inamilikiwa na mtu mwingine,” alisema diwani huyo wa Kata ya Mchangani.

Diwani wa Ligoma, Abdallah Zubeir alisema katika mfumo wa awali ilikuwa rahisi kuwafikia viongozi wa Amcos malipo yalipocheleweshwa na kuonyesha wasiwasi kama jambo hilo litakuwa rahisi katika mfumo mpya.

Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Simon Chacha alisema mfumo huo unalenga kushughulikia changamoto ambazo wakulima walikabiliana nazo katika misimu mingi iliyopita ya uuzaji koroshoa, “Sioni kama kuna tatizo katika usimamizi, wilaya yangu itasimamia kikamilifu mabadiliko hayo.”

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Alfred Francis alisema mwaka jana mfumo huo ulipingwa na vyama vya ushirika, akiomba ushirikiano wa wilaya kuhakikisha unatekelezwa kwa mafanikio kwani unalenga kutoa suluhisho la malipo kwa wakulima.

Meneja Mkuu wa Tamcu, Marcelino Mrope aliesema maandalizi ya msimu wa 2024/25 unaotarajia kuanza Oktoba 29, 2024, wilayani humo umefikia asimilia 70.

Alisema Tamcu iko tayari kutumia mfumo mpya katika kuwalipa wakulima katika msimu wa 2024/25, badala ya Amcos.

“Tamcu imefanya mafunzo kuhusu mfumo mpya kwa kuwaalika viongozi wa chama cha ushirika cha Lindi Mwambao na maofisa wa ushirika kutoka mkoani Lindi ili kuwajengea uwezo viongozi na wasimamizi wa Amcos za Tunduru, maofisa wa ushirika na wasimamizi wa Tamcu,” alisema na kubainisha kuwa mafunzo hayo yalifanyika Ijumaa, Septemba 20, 2024.

Alisema katika msimu wa 2024/25, Tamcu inatarajia kuzalisha tani 28,000 za korosho ghafi, takriban tani 2,000 zaidi ya tani 26,062.3 zilizozalishwa katika msimu wa 2023/24.