Dar es Salaam. Baraza la Sanaa Taifa (Basata) chini ya Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk Kedmond Mapana, leo Aprili 17, 2025 limefanya kikao na Miss Tanzania 2023, Tracy Nabukeera pamoja na Mkurugenzi wa Kampuni ya Look, Basila Mwanukuzi kwa ajili ya kusuluhisha tofauti zao.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Basata inaeleza kuwa lengo la kuwaita wawili hao ni kuhusiana na suluhu iliyotokana na Tracy ambaye amejitoa kwenye mashindano Kimataifa.
“Kikao hicho kimefanyika katika ofisi za BASATA kwa lengo la kujadili na kutafuta muafaka juu ya sintofahamu na changamoto zilizojitokeza baina ya pande hizo mbili. Kufuatia tangazo rasmi la Tracy la kujiondoa kwenye mashindano ya Miss World 2025,” imeeleza taarifa hiyo
Aidha iliendelea kwa kueleza “Kikao hiki cha usuluhishi kinatazamwa kama hatua muhimu katika kurejesha maelewano na kuhakikisha mustakabali mzuri wa tasnia ya urembo nchini Tanzania,”
Utakumbuka kuwa kupitia ukurasa wa Instagram wa Tracy April 14, 2025 alichapisha ujumbe ambao ulizua mijadala katika mitandao ya kijamii akidai amejiondoa kushiriki Miss World 2025 kutokana na kukosa ushirikiano

Hata hivyo baada ya madai hayo Mwananchi ilimtafuta Mkurugenzi wa Kampuni ya Look inayoendesha mashindano ya kumsaka Miss Tanzania, Basila Mwanukuzi na kusema Tracy hajajitoa kushiriki Miss World 2025 kwani sio yeye aliyekuwa amepangwa kwenda kushiriki.
“Mwaka jana alituandikia barua kuwa anapitia changamoto binafsi. Kwa hiyo tulikuwa tunamlinda hatukutaka kutangaza kuwaambia watu kuwa anapitia changamoto.

“Itoshe tu kusema hajajitoa kwa sababu alikuwa haendi kutokana na hizo changamoto alizosema anazipitia na alishukuru kwa sapoti na nafasi aliyopata kama Miss Tanzania. Sisi hatukutaka kumbebesha lawama, tulimpa muda kwa sababu alikuwa anapitia namna ya kutatua changamoto yake,” alisema Basila