Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amemwandikia barua Mwenyekiti wa Baraza la Usalama na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kufuatia mashambulizi ya jana ya utawala wa Kizayuni dhidi ya vituo vya kijeshi vya Iran na kusisitiza kuwa: Hatua za Tel Aviv ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa kimataifa.
Sayyid Abbas Araqchi amesema katika barua aliyomwandikia Pascal Christian Mwenyekiti wa Baraza la Usalama na Antonio Guterres Katibu Mkuu wa UN kwamba: Utawala wa kigaidi wa Israel mapema jana Jumamosi ulitekeleza mashambulizi ya kijeshi ya anga katika maeneo kadhaa katika mikoa ya Khuzistan, Ilam na kando ya mji wa Tehran.
Araqchi ameongeza kuwa: Maafisa wa jeshi wanne wa Iran wameuawa shahidi ingawa mfumo wa ulinzi wa anga wa Iran ulinasa aghalabu ya makombora ya utawala wa Kizayuni.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kuwa lau mfumo wa ulinzi wa anga wa Iran ungeshindwa kuzuia mashambulizi ya utawala wa Kizayuni, hujuma ya jana ya utawala huo ingesababisha maafa makubwa.

Amesema, hujuma haramu za utawala wa Israel zimekiuka msingi wa sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa hususan kifungu cha 2 cha kipengee cha 4 cha mkataba huo ambacho kinaeleza wazi kuwa ni marufuku kutumiwa nguvu dhidi ya mamlaka ya kujitawaka na umoja wa ardhi nzima ya nchi yoyote.