Barrick kutoa leseni zake kwa wananchi kudhibiti uvamizi

Tarime. Mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara uliopo Nyamongo wilayani Tarime Mkoa wa Mara unatarajia kutoa leseni zake nne za uchimbaji na kuwapa vijana kwa ajili ya kuanzisha shughuli za uchimbaji wa dhahabu.

Hatua hiyo mbali na kulenga kuimarisha uchumi wa vijana pia unatarajiwa kuwa suluhisho la  kudumu juu ya vitendo vya uvamizi wa mgodi unaofanywa na baadhi ya vijana mara kwa mara mgodini hapo kwa lengo la kuiba mawe yenye dhahabu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 12,2025 kuhusu miradi ya maendeleo inayotekelezwa na mgodi huo, Meneja Mkuu wa Barrick North Mara,  Apolinary Lyambiko amesema uamuzi huo unatokana na makubaliano baina ya mgodi na serikali ambapo tayari Waziri wa Madini ameunda kamati kwaajili ya kufanikisha suala hilo.

“Tayari tumetoa leseni mbili na tunatarajia kutoa zingine mbili, kwa sasa kamati iliyoundwa na waziri inafanya kazi ya kufanya upembuzi yakinifu juu ya namna ambavyo uchimbaji huo utafanyika ikiwa ni pamoja na namna ya kugawa vitalu hivyo kwa vijana na wanufaika watapatikanaje pamoja na mambo mengine ili kuwa na tija,” amesema.

Meneja Mkuu wa Mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara uliopo wilayani Tarime Mkoa wa Mara, Apolonary Lyambiko akizungumza na waandishi wa habari juu ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya jamii inayotekelezwa na mgodi huo. Picha na Beldina Nyakeke

Lyambiko amesema katika makubaliano hayo, mgodi pamoja na serikali watatoa gharama za awali ili kufanikisha uchimbaji huo na hivi sasa kamati hiyo ambayo inahusisha wataalamu kutoka ofisi mbalimbali ikiwepo ofisi ya Ofisa madini Mkoa, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST) pamoja na taasisi zingine ipo katika hatua za mwisho kukamilisha upembuzi huo ingawa hakusema kazi hiyo itakamilika lini.

Amesema vitendo vya uvamizi vinavyofanywa  na baadhi ya vijana kwa lengo la kuiba mawe ya dhahabu mgodini hapo vimeanza kurejea baada ya kukomeshwa kwa kipindi cha nyuma na kwamba anaamini vijana watakapoanza kuchimba dhahabu vitendo hivyo vitaisha kabisa.

“Baada ya jitihada mbalimbali zilizofinywa na serikali pamoja na mgodi vitendo hivi vilipungua sana kiasi kwamba tulikuwa tunamaliza wiki nzima bila kuwepo kwa tukio hata moja ila kwa sasa vimeanza kurejea hasa msimu huu wa mvua ambapo kila mvua inaponyesha lazima kunakuwepo na uvamizi,” amesema

Kuhusu utekelezaji wa miradi itokanayo  na fedha uwajibikaji wa kampuni kwa wananchi (CSR) mgodi huo umetenga zaidi ya Sh4.7 bilioni zilizotokana na uzalishaji mwaka 2024 fedha ambazo zinatarajiwa kutumika mwaka huu kwaajili ya miradi ya maendeleo ya jamii.

Amesema hivi sasa kazi ya kuibua miradi itakayotekelezwa na fedha hizo inaendelea katika vijiji husika huku miradi hiyo ikitarajiwa kuwa katika sekta za afya, elimu, maji, ujasiriamali na miundombinu.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa miradi mingine ya CSR unaendelea katika kata 26 za halmashauri ya Wilaya ya Tarime vijijini baada ya mgodi huo kutoa zaidi ya Sh9 bilioni zilizotokana na uzalishaji wa mwaka 2023 kwaajili ya shughuli hizo.

Baadhi ya wakazi wa Nyamongo wameupongeza mgodi kwa uamuzi huo wa kutoa leseni kwaajili ya vijana kuanza uchimbaji hivyo kuomba mchakato huo ufanyike kwa haraka ili vijana waanze uzalishaji.

John Marwa amesema uamuzi huo pamoja na kuinua uchumi wa vijana na jamii kwa ujumla pia utasaidia kuimarisha mahusiano kati ya mgodi na jamii hivyo mgodi huo kuwa na nafasi ya kutekeleza majukumu yake kwa usalama na amani zaidi.

“Tunaomba tu kusiwepo na ubaguzi kwenye ugawaji wa hivyo vitalu pia kamati ifanye mchakato huo haraka ili kuruhusu vijana kuanza kuchimba kwani hili ni hitaji la vijana kwa muda mrefu sana,” amesema

Nyangi Ghati amesema anaamini vijana wa kike pia watapewa fursa  wakati wa ugawaji wa vitalu huku akiamini kuwa kuanza kwa uchimbaji huo kutakuwa ni suluhisho la kudumu juu ya vitendo vya uvamizi katika mgodi.

“Mara nyingi nyakati za kuelekea uchaguzi kama sasa uvamizi unaongezeka sana kwani suala hili pia huwa linahusishwa na mambo ya kisiasa sasa kama vijana watapewa maeneo yao ili wachimbe ni dhahiri hakutakuwa na uvamizi kabisa mgodini,” amesema

Mwita Wesiko ambaye mdogo wake alifariki kwa kupigwa risasi baada ya kutokea fujo zilizosababishwa na uvamizi mgodini amesema uchimbaji huo wa vijana unapaswa kuwa endelevu hatua ambayo itapelekea vijana kuwa imara kiuchumi na kuachana na vitendo vya kiuhalifu kama uvamizi.

“Sio kwamba vijana huku ni wakorofi ila haya mambo huwa yanatokana na ukweli kuwa  shughuli kuu ya hapa ni uchimbaji wa madini na vijana hawana maeneo ya kuchimba hivyo wengine wanaona njia iliyopo ni kuingia mgodini na kuchukua mawe,” amesema

Vitendo vya uvamizi katika mgodi huo vimekuwa vikitokea mara kwa mara ambapo baadhi ya vijana wamekuwa wakidaiwa kuvamia mgodi na kisha  kupora mali  ikiwepo mawe yenye dhahabu huku chanzo kikidaiwa kuwa ni hali mgumu ya maisha.

Vitendo hivyo ambavyo vimekuwa vikifanyika kwa muda mrefu vimekuwa na athari nyingi ikiwepo uharibifu wa mali pamoja na majeruhi na vifo vitakanavyo na mapigano kati ya wavamizi na askari pamoja na walinzi wa mgodi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *