Baresi akiri anastahili ‘thank you’

SAA chache baada ya uongozi wa Mashujaa kuvunja benchi lao la ufundi, aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mohamed Abdallah ‘Bares’ amesema wamewajibika kutokana na matokeo mabovu ya timu hiyo.

Baada ya kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Singida Black Stars, uongozi wa Mashujaa ulitoa taarifa ya kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba na kocha huyo, kocha wa viungo Hussein Bunu na kocha wa makipa Rafael Nyendi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Baresi alisema ameridhia kuachana na timu hiyo kutokana na matokeo mabaya na yeye kama kocha anatakiwa kuwajibika kwa hilo licha ya kufanya kazi yake kwa usahihi.

“Tumefanya majukumu yetu kama inavyotakiwa, nikweli tyulikuwa bora mzunguko wa kwanza lakini tumeshindwa kuendeleza ubora wetu mzunguko wa pili hivyo kwa kuwa kocha ndio anatakiwa kuwajibishwa kutokana na matokeo mabaya nimeridhia kuondoka,” alisema Baresi na kuongeza;

“Matokeo mabaya tuliyokuwa tunayapata ni sehemu ya mchezo nafikiri ni upepo mbaya tulikuwa tunaupitia naamini wachezaji watapambana kwenye mechi zilizobaki kuipambania Mashujaa isishuke daraja nawatakia kila la kheri.”

Baresi alijiunga na Mashujaa msimu uliopita siku chache baada ya kupanda daraja hivyo ameifundisha kwa msimu mmoja na nusu, msimu wa kwanza 2023/24 aliiongoza timu hiyo ikimaliza nafasi ya nane kwenye msimamo.

Msimu huu ameiongoza kwenye mechi 22, ameshinda tano, sare nane, vipigo tisa, timu imefunga mabao 17 ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara 26 ameifanya ikusanye pointi 23 na kuwa nafasi ya 11 kwenye msimamo.