Barcelona imefanikiwa kubeba Ubingwa wa Ligi Kuu Hispania maarufu kama “La Liga” mara baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wapinzani wao Espanyol katika mchezo uliochezwa jana kwenye Uwanja wa RCDE.

Kwa ushindi huo, Barcelona imefikisha pointi 85 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote, huku wapinzani wao wakubwa, Real Madrid wakishika nafasi ya pili kwa pointi 78, kila mmoja akiwa amecheza mechi 36.
Baada ya kuwafunga mahasimu wao Real Madrid wikiendi iliyopita Barcelona walihitaji kupata pointi tatu katika michezo mitatu iliyobakia ili watangaze ubingwa wa La Liga msimu huu.

Katika mchezo wa jana ilisubiriwa kwa dakika 53 ambapo ilishuhudiwa mshambuliaji, Lamine Yamal akiandika bao la kuongoza na kuipa Barcelona matumaini ya kutwaa ubingwa msimu huu.
Fermín López aliihakikishia Barcelona kutangaza ubingwa baada ya kufunga bao la pili katika dakika za mwishoni mwa mchezo akimalizia pasi ya mfungaji wa bao la kwanza Lamine Yamal.

Baada ya kupata ushindi huo, Barcelona wamekuwa Mabingwa wa La Liga kwa mara ya 28 wakiwa nyuma ya mahasimu wao Madrid wanaoongoza wakiwa na mataji 36. Mara ya mwisho Barcelona ilibeba taji hilo msimu wa 2022-2023, ilipokuwa chini ya kocha, Xavi Hernandez.
Mara baada ya Barcelona kutwaa ubingwa huo, Real Madrid ambao walikuwa mabingwa wa msimu uliopita wa 2023-24, waliwapongeza wapinzani wao kwa kutwaa taji hilo.

Kupitia kurasa zake zote za mitandao ya kijamii, Real Madrid waliandika ujumbe mfupi uliosema: “Hongera Barcelona kwa kutwaa ubingwa wa La Liga msimu wa 2024-25.”
Katika msimu wa 2024-25, FC Barcelona ilikutana na Real Madrid mara nne kwenye mashindano mbalimbali, na kushinda mechi zote hizo. Hii ni mara ya kwanza katika historia ya kisasa kwa Barcelona kushinda kila “El Clásico” ndani ya msimu mmoja.

Ikumbukwe Barcelona inayoongozwa na kocha, Hansi Flick msimu wa 2024-2025 katika mechi nne walizokutana na Real Madrid ilishinda zote, ikiwa ni pamoja na michezo miwili ya La Liga, fainali ya Supercopa na fainali ya Copa del Rey.
Barcelona imesalia na michezo miwili ya Ligi Kuu nchini Hispania ambapo Mei 18 itakuwa kwenye Uwanja wa Olimpic Luis Companys kukabiliana na manyambizi wa njano Villarreal kabla ya kwenda Bilbao, Mei 25 mwaka huu kufunga pazia la La Liga msimu huu kwenye Uwanja wa San Mamés dhidi ya wenyeji Athletic Club.