Barcelona yashinda, yarudi kileleni La Liga

Barcelona, Hispania. Barcelona imefanikiwa kurudi kwenye kilele cha Ligi Kuu Hispania maarufu kama La Liga, baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Rayo Valecano katika mchezo uliochezwa usiku wa kuamkia leo kwenye Uwanja wa Lluís Companys Olympic.

Barcelona imerudi kileleni baada ya siku 58, tangu iliposhushwa Desemba 21, 2024 baada ya kufungwa na Atletico Madrid ambayo iliongoza ligi kwa muda kabla ya Real Madrid kupanda juu.

Bao pekee la Barcelona lilifungwa na mshambuliaji, Robert Lewandowski kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 28, baada ya kiungo wa Rayo Valecano, Pathé Ciss kumchezea vibaya beki wa Barcelona, Iñigo Martínez alipokuwa akiwania mpira ndani ya eneo la hatari.

Baada ya ushindi dhidi ya Rayo Valecano, Barcelona sasa imefikisha pointi 51 sawa na mahasimu wao Real Madrid huku tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa ikiwabeba Barcelona.

Barcelona mpaka sasa imefunga mabao 65 na kuruhusu 25, wakati Real Madrid yenyewe imefunga mabao 52 na kuruhusu 23.

Sare ya bao 1-1 waliyoipata Madrid Jumamosi dhidi ya Osasuna huku Atletico nayo ikibanwa mbavu na Celta Vigo kwa sare ya bao moja kwa moja ilirahisisha mambo kwa Barcelona ambayo ilitakiwa kupata matokeo ya ushindi ili kukaa kileleni.

Bao alilofunga mshambuliaji Lewandowski linakuwa la 20 katika msimu huu ndani ya La Liga akiwa ndiyo kinara wa mabao mpaka sasa akifuatiwa na Kylian Mbappe wa Real Madrid mwenye mabao 17.

Mchezo unaofuata Barcelona itakuwa ugenini kukabiliana na Las Palmas, Februari 22, 2025 katika mbio za kuwania Ubingwa wa La Liga huku mahasimu wao Real Madrid nao watakuwa ugenini kuvaana na Girona Februari 23, 2025.