Barcelona, PSG zafuzu nusu fainali Ulaya kwa vichapo

Barcelona na PSG zimetinga hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya licha ya kupokea vichapo katika mechi zao jana usiku dhidi ya Borussia Dortmund na Aston Villa.

Ushindi wa tofauti kubwa ya mabao ambao kila moja ilipata nyumbani umeonekana kuzisaidia PSG na Barcelona ambazo jana zilijikuta zikipata wakati mgumu katika viwanja vya ugenini.

Kwenye Uwanja wa Signal Iduna Park, wenyeji Borussia Dortmund waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Barcelona lakini wakajikuta wakiaga kwa kichapo cha jumla cha mabao 5-3 kwa vile mechi ya kwanza ambayo walikuwa ugenini Hispania, walifungwa mabao 4-0.

Mabao yote matatu ya Borussia Dortmund katika mchezo wa jana yamefungwa na Serhou Guirassy na bao la Barcelona lilikuwa la kujifunga la Ramy Bensebaini.

Kwa kufuzu huko, Barcelona inatinga hatua ya nusu fainali kwa mara ya kwanza ndani ya misimu sita tangu msimu wa 2018/2019.

Serhou Guirassy amekuwa mchezaji wa nne wa Borussia Dortmund kufunga mabao matatu katika mchezo mmoja wa Ligi ya Mabingwa Ulaya akifuata nyayo za Pierre-Emerick Aubameyang, Robert Lewandowski na Karim Adeyemi.

Huo umekuwa ushindi wa kwanza kwa Borussia Dortmund dhidi ya Barcelona katika mashindano ya Ulaya ambapo katika mara sita za nyuma, ilipoteza nne na kutoka sare mbili.

Borussia Dortmund imefungwa mabao nane na Barcelona msimu huu, idadi ambayo ni kubwa zaidi kwa timu hiyo kufungwa ndani ya msimu mmoja kwenye mashindano hayo ndani ya msimu mmoja.

Katika Uwanja wa Villa Park, Aston Villa imeibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya PSG lakini haukutosha kuivusha kwenda nusu fainali kwa vile ilipoteza kwa mabao 3-1 katika mechi ya kwanza ugenini.

Mabao ya Aston Villa katika mechi ya jana yamefungwa na Youri Tielemans John McGinn na Ezri Konsa huku yale ya PSG yakipachikwa na Achraf Hakimi na Nuno Mendes.

Hii ni mara ya kwanza baada ya miaka 24 kwa PSG kupoteza mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuongoza kwa mabao mawili ambapo mara ya mwisho ilifanya hivyo mwaka 2001 ilipofungwa mabao 4-3 na Deportivo la Coruna.

Katika nusu fainali, PSG inangojea mshindi wa jumla baina ya Real Madrid na Arsenal zinazocheza leo Jumatano, Aprili 16 na Barcelona inangojea timu itakayofuzu baina ya Inter Milan na Bayern Munich ambazo nazo zinacheza leo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *