Barcelona, Inter zatoshana nguvu

Barcelona imelazimishwa sare ya mabao 3-3 nyumbani na Inter Milan, matokeo yanayoifanya mechi ya marudiano baina yao kuwa wazi katika mbio baina ya timu hizo kuisaka fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.

Katika mchezo huo wa nusu fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baina yao uliochezwa kwenye Uwanja wa Olímpic Lluís Companys jijini Barcelona, wenyeji walilazimika kutoka nyuma mara mbili na kusawazisha mabao baada ya kutanguliwa.

Mapema tu dakika ya kwanza, Inter ilipata bao la utangulizi kupitia kwa Marcus Thulam na dakika 20 baadaye ikapata la pili kupitia kwa Denzel Dumfries.

Barcelona ilijibu kwa haraka kupitia mabao ya Lamine Yamal katika dakika ya 24 na lingine la Ferran Torres katika dakika ya 38 na kufanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa sare ya mabao 2-2.

Dakika ya 64, Dumfries aliitanguliza tena Inter lakini lilidumu kwa dakika moja tu kwani Barcelona walisawazisha dakika ya 65 baada ya kipa Yann Sommer kujifunga alipokuwa katika harakati za kuokoa shambulizi la wenyeji.

Sare hiyo imefanya mechi hiyo kuingia katika rekodi ya kuwa mechi ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyozalisha mabao mengi ambayo awali ilikuwa inashikiliwa na mchezo baina ya Dynamo Kyiv na Bayern Munich uliomalizika kwa sare ya mabao 3-3 msimu wa 1998/1999.

Imekuwa ni mara ya tatu kwa Inter Milan kushindwa kupata ushindi katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya licha ya kuongoza kwa mabao mawili au zaidi.

Lamine Yamal ameweka rekodi ya kuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufunga bao katika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akifanya hivyo katika umri wa miaka 17 na siku 291.

Timu hizo zitarudiana katika Uwanja wa Giuseppe Meazza, wiki ijayo, Mei 6, 2025 ambapo mshindi atakutana na mshindi wa mechi baina ya PSG na Arsenal kucheza fainali.

Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu imepangwa kufanyika katika Uwanja wa Allianz Arena, Ujerumani, Mei 31 mwaka huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *