Barcelona, Inter Milan mechi ya kisasi leo

Barcelona, Hispania. Barcelona itaikaribisha Inter Milan katika mchezo wa kwanza wa nusu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya utakaochezwa leo Aprili 30, 2025 katika Uwanja wa Olympic Luis, Cataluña.

Barcelona ambayo imetoka kuchukua taji la Kombe la Mfalme Jumamosi iliyopita kwa kuwafunga mahasimu wao Real Madrid mabao 3-2 leo itakuwa na kibarua kingine cha kuhakikisha wanapata matokeo mazuri dhidi ya Inter Milan ili kujiweka pazuri kufuzu katika fainali ya mashindano hayo.

Haitakuwa mechi rahisi kwani Inter Milan wataingia kuhakikisha nao wanapata matokeo mazuri baada ya kutoka kupoteza mechi tatu mfululizo kwenye Ligi Kuu ya Italia ‘Seria A’.

Inter inaingia kwenye mechi ya leo ikiwa na safu nzuri ya ulinzi kwani katika michezo 12 ya Ligi ya Mabingwa Ulaya imeruhusu mabao matano huku yenyewe ikifunga 19 ambapo imeshinda mechi tisa, imepata sare mechi mbili na kupoteza mechi moja.

Barcelona imecheza mechi 12 hadi sasa ikiwa imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 17 huku yenyewe ikifunga mabao 37 ambapo imeshinda mechi tisa, imepata sare moja na kupoteza mechi mbili.

Mchezo wa fainali ya Kombe la Mfalme waliocheza Barcelona dhidi ya Madrid unaweza kuwafanya wachezaji waingie na uchovu kutokana na nguvu kubwa waliotumia mpaka kuwashinda Madrid, lakini kocha wa Barcelona, Hansi Flick amesema kwamba wachezaji wake wako fiti kwa mchezo wa leo.

“Wachezaji wako vizuri, kuhusu mchezo uliopita ni kama umetuongezea hamasa ya kuendelea kupata matokeo mazuri. Tuko tayari kukabiliana na Inter na malengo yetu ni kufika fainali,” amesema Flick.

Katika mchezo wa leo Barcelona itawakosa baadhi ya nyota wake ambao wameripotiwa kuwa nje ya kikosi kutokana na kusumbuliwa na majeraha. Baadhi yaO NI mshambuliaji, Robert Lewandowski, Marc Casado, Marc Bernal pamoja na Alejandro Balde.

Wakati wachezaji hao wakiripotiwa kuwa nje ya kikosi cha Barcelona, golikipa namba moja wa timu hiyo Marc-André ter Stegen amerejea kikosini baada ya kuwa nje kwa muda mrefu alipokuwa akisumbuliwa na majeraha ya goti tangu alipoumia Septemba mwaka jana.

Hata hivyo, Hansi Flick hajathibitisha kumtumia kipa huyo kwenye mchezo wa leo huku Wojciech Szczęsny akipewa nafasi kubwa ya kuanza kwenye milingoti mitatu dhidi ya Inter Milan.

“Ter Stegen atakuwa kwenye kikosi dhidi ya Inter Milan, nadhani tutamfanyia mabadiliko kwenye La Liga. Szczęsny atacheza kwenye Ligi ya Mabingwa,” amesema Flick.

Kwa upande wa Inter Milan wao watamkosa beki, Benjamin Pavard ambaye atakuwa nje ya kikosi cha Simone Inzaghi kutokana na kukabiliwa na majeraha ya kifundo cha mguu.

Timu hizi zimekutana mara 12 ambapo Barcelona imeshinda mechi sita, sare mara nne huku Inter Milan ikishinda mara mbili.

Mara ya mwisho timu hizi zilikutana kwenye hatua ya makundi mwaka 2023 ambapo Inter Milan ilipata ushindi ikiwa nyumbani huku ikiilazimisha Barcelona sare ya mabao 3-3 kwenye uwanja wa Nou Camp.

Mara ya mwisho timu hizi kukutana kwenye hatua ya nusu fainali ilikuwa mwaka 2010 ambapo ilishuhudiwa Barcelona ikitolewa na Inter Milan kwa tofauti ya mabao 3-2 kwani katika mchezo wa kwanza uliochezwa Aprili 20, 2010 Inter Milan ilipata ushindi wa mabao 3-1 kabla ya kwenda ugenini ilipofungwa bao 1-0 Aprili 28, 2010.

Baada ya kuiondoa Barcelona kwenye michuano hiyo Inter Milan ilibeba Ubingwa wa UEFA kwani iliifunga Bayern Munich mabao 2-0 katika mchezo wa fainali uliochezwa Mei 22, 2010 kwenye uwanja wa Santiago Bernabeu, Hispania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *