Barca hatarini kunyang’anywa pointi, chanzo hiki hapa

Barcelona ipo kwenye hatari ya kupokwa pointi baada ya sasa kufanyiwa uchunguzi juu ya kucheza mchezaji asiyestahili kwenye mechi ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Osasuna kwenye La Liga, Alhamisi iliyopita.

Osasuna imewasilisha malalamiko kwenye chama cha soka cha Hispania juu ya Barcelona kumchezesha mchezaji ambaye hakupaswa kutumika kwenye mechi hiyo, beki wa kati Inigo Martinez.

Martinez, 33, alicheza dakika zote 90 katika mechi hiyo ya LaLiga licha ya kwamba alijiondoa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Hispania wiki iliyopita.

Beki huyo wa zamani wa Athletic Bilbao na Real Sociedad alijiondoa kwenye kikosi cha La Roja kinachonolewa na Luis de la Fuente baada ya taarifa ya kidaktari kutoka kwa Barcelona iliyodai mchezaji huyo anasumbuliwa na maumivu ya goti, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na timu ya taifa ya Hispania. Nafasi ya Martinez kwenye kikosi cha La Roja ilichukuliwa na Dean Huijsen wa Bournemouth baada ya kuondoka kikosini ni mgonjwa.

Madai ya Osasuna ni Martinez kitendo cha kucheza mechi ya La Liga amevunja kanuni ya Fifa kifungu namba 5, inayosema mchezaji yeyote anayejiondoa kwenye timu ya taifa kwa madai ni majeruhi, hatakiwi kuichezea timu yake ya klabu kwa siku zinazofuatia baada ya timu yake ya taifa kucheza mechi  labda tu kama kutakuwa na makubaliano na shirikisho la soka la nchi husika.

Hilo linaweza kumweka kwenye matatizo Martinez, ambaye alitumika kwenye mechi dhidi ya Osasuna ikiwa imepita siku nne tu baada ya Hispania kucheza mechi ya pili ya Nations League dhidi ya Uholanzi, Jumapili, iliyopita.

Hivyo, Barcelona inakabiliwa na adhabu endapo ikigundulika imefanya makosa kwenye hilo. Kupokwa pointi au kugeuzwa kwa matokeo ya mechi hiyo kwenda kwa wapinzani ni kitu kinachoweza kutokea kama adhabu ya tukio hilo.

Jambo hilo linaweza kutibua kwa namna fulani msimu wa Barcelona, ambapo ushindi huo wa Osasuna uliwafanya kujikita kileleni kwenye msimamo wa La Liga kwa tofauti ya pointi tatu dhidi ya mahasimu wao Real Madrid.

Osasuna, kwa upande wao wanahitaji pointi kwa nguvu zote kwa sababu mechi hiyo iliwafanya wawe juu kwa pointi moja tu kutoka kwenye shimo la kushuka daraja. Bado haijafahamika kama chama cha soka cha Hispania kilitoa ruhusa kwa Martinez kujitoa kwenye kambi ya timu ya taifa nakucheza mechi hiyo. 

Barcelona na Osasuna zilipewa muda usiozidi wiki moja kujiandaa na mechi hiyo baada ya ratiba yao ya awali kuahirishwa, ambapo mwanzoni ilitakiwa kufanyika Machi 8, lakini iliahirishwa baada ya kifo cha ghafla cha daktari wa timu ya Barcelona, Carles Minarro Garcia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *