Baraza la Mawaziri Tanzania sasa kidijitali

Dodoma. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa Baraza la Mawaziri utasaidia kuboresha utendaji kazi na kuleta ufanisi zaidi katika kuwahudumia wananchi.

Amesema maboresho hayo ya matumizi ya mfumo wa kielektroniki yatasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza matumizi ya karatasi katika vikao vya Serikali, hususan Baraza la Mawaziri, hivyo kupunguza changamoto ikiwemo kuchelewa kwa taarifa, gharama kubwa za uchapaji na hatari ya upotevu wa taarifa muhimu.

Amesema hayo leo Jumatatu, Novemba 11, 2024 wakati akifunga mkutano wa kazi wa mawaziri na naibu mawaziri kuhusu matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa Baraza la Mawaziri (e-Cabinet), kwenye ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma.

Ameongeza kuwa hatua hiyo inatokana na jitihada na malengo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kusisitiza umuhimu wa mawaziri na watumishi wa umma kuzingatia mabadiliko ya kiteknolojia katika utendaji kazi.

“Matokeo ya mwaka 2023 ya ulinganifu baina ya nchi katika muktadha wa ukomavu wa matumizi ya teknolojia serikalini (Government Technical Maturity Index), nchi yetu ilishika nafasi ya tatu, ikilinganishwa na nchi nyingine barani Afrika.

“Tunampongeza na kumtakia kila la kheri Rais Samia aendelee kubuni zaidi kwa manufaa ya Taifa letu.”

Taarifa kwa umma iliyotolewa na ofisi ya Waziri Mkuu imeeleza kuwa Majaliwa amesema mkutano huo kuhusu matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa Baraza la Mawaziri ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha mawaziri na watumishi wa umma wanakuwa na ujuzi wa kisasa wa uendeshaji wa shughuli za Serikali na utumishi kwa ujumla.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema uanzishwaji wa mfumo huo wa kielektroniki ni utekelezaji wa Ibara za 102 na 103 za Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 zinazoelekeza Serikali kuhakikisha kuwa sayansi, teknolojia na ubunifu vinatumika kikamilifu kuendesha sekta za kukuza uchumi kwa lengo la kufikia uchumi wa hadhi ya kipato cha kati ambao ni shindani, jumuishi na unaoongozwa na viwanda.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amewapongeza wataalamu kutoka Wakala wa Serikali Mtandao kwa kufanikisha mafunzo hayo.

Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema mafunzo hayo ni mwendelezo wa mpango wa Serikali kwenda kwenye matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa Baraza la Mawaziri (e-Cabinet) mchakato uliokuwa wa muda mrefu kupitia wataalamu wa Wakala wa Serikali Mtandao.