Baraza la Kiislamu la Msumbiji lajitolea kupatanisha baina ya serikali na waasi

Baraza la Kiislamu la Msumbiji limejitolea kuwa mpatanishii kati ya serikali na waasi wanaopigana na serikali katika jimbo la kaskazini la Cabo Delgado katika taifa hilo la kusini mwa Afrika.

Wakati wa mkutano wa kimataifa katika mji mkuu Maputo siku ya Jumanne, viongozi hao wa Kiislamu walieleza kuwa mzozo unaoendelea katika eneo lenye utajiri wa gesi la Cabo Delgado umevuruga eneo zima na kusababisha ” jinamizi miongoni mwa watu.”

Msemaji wa Kongamano hilo Mussa Suede amesema baraza hilo liko tayari kuleta amani katika mkoa huo kwa njia ya mazungumzo.

Amesema kuwa kila juhudi zinafanyika ili Waislamu katika taifa hilo la kusini mwa Afrika “wawe na misimamo ya wastani kwani Uislamu ni dini ya amani.”

Uasi wa kutumia silaha, ambao chimbuko lake limedaiwa kuwa ni umasikini, ulikumba kaskazini mwa Msumbiji mwaka 2017, na kusababisha maelfu ya watu kupoteza maisha na wengine kuyahama makazi yao. Shirika la nishati la Ufaransa la TotalEnergies linachimba gesi nchini Msumbuji na linatuhumiwa kupora utajiri wa nchi hiyo huku wakazi wakibakia kuwa masikini.

Mwaka huu, zaidi ya watu 80,000 wamekimbia makazi yao kufuatia mashambulizi kutoka kwa makundi yenye silaha.