Baqaei: Mashinikizo haramu ya Marekani dhidi ya watu wa Iran yameendelea hadi leo

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani sera na mienendo ya kindumakuwili ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ismail Baqaei ameashiria uungaji mkono wa pande zote wa Marekani kwa utawala wa Saddam katika vita vya kulazimishwa miaka minane dhidi ya Iran na kusema kuwa, mashinikizo haramu na ya kikatili ya Marekani dhidi ya taifa la Iran yameendelea hadi leo.

Baqaei amesema hayo katika ujumbe aliouandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X na kubainisha kwamba: Mashinikizo haramu na ya kidhalimu ya Marekani, na vilevile uungaji mkono wa nchi hiyo kwa utawala wa dikteta Saddam katika vita vya miaka 8 vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran, ikiwa ni pamoja na vikwazo haramu.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza kuwa, wananchi wa Iran hawawezi kusahau historia ndefu na nyeusi ya uingiliaji haramu na uvunjifu wa amani wa Marekani nchini Iran, hususan mapinduzi ya Marekani na Uingereza ya Agosti 1953, ambayo yaliipindua serikali ya kwanza iliyochaguliwa na wananchi wa Iran na kurejesha udikteta wa kifalme.