Banduka kuzikwa leo Ugweno Kilimanjaro

Moshi. Mwili wa Mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania, Nicodemus Banduka (80)  utazikwa leo Jumatano Februari 12, 2025  katika makaburi ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mruma, Ugweno, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro.

Banduka ambaye aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi  ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na serikalini amefariki dunia Februari 7, 2025.

Akizungumza na Mwananchi, msemaji wa familia ambaye ni mtoto wa marehemu, Manase Banduka amesema  wanatarajia kumzika baba yao leo Jumatano katika Usharika wa KKKT Mruma.

Amesema viongozi mbalimbali wa chama na Serikali wanatarajiwa kushiriki katika maziko hayo ambayo yatafanyika katika makaburi ya kanisa.

“Tutamzika baba kesho (leo) na ndiyo tuko njiani kuelekea Ugweno Kilimanjaro, Kijiji cha Mruma.Mpaka sasa hatujapata taarifa ni viongozi gani watashiriki msiba huo ila tunafahamu viongozi wa chama na serikali watakuwepo lakini hatujajua ni nani na nani atakuja,” amesema Manase.

Akizungumzia ratiba, Manase amesema, asubuhi wataanza shughuli za maombolezo nyumbani na saa 6:30 mchana msafara utaondoka kuelekea kanisani kwa ajili ya ibada na maziko.

“Kesho (leo) asubuhi kutakuwa na shughuli kidogo nyumbani kisha  tutaelekea kanisani KKKT Usharika wa Mruma, ambapo saa 7:00 mchana ibada itaanza na atazikwa kwenye makaburi ya Kanisa usharika wa Mruma.”

Juzi akizungumzia kifo cha mwanasiasa huyo, Mbunge wa Mwanga (CCM), Joseph Tadayo, amesema mzee Banduka alikuwa mmoja wa wanasiasa wakongwe kutoka Wilaya ya Mwanga na atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa alioutoa serikalini na kwenye chama.

Thadayo amesema Mzee Banduka atakumbukwa kama kada mbobezi na mtiifu wa CCM aliyekuwa na uwezo mkubwa wa kuzielewa na kuzinadi sera za CCM.

“Aliaminika sana na Baba wa Taifa kama Kada wa CCM, na alikuwa na kipawa kikubwa cha kuhimiza maendeleo, na amekiwa kiongozi katika nyadhifa mbalimbali na mwaka 2005, alijitokeza kuomba uteuzi kwa nafasi ya ubunge wa Jimbo la Mwanga lakini kura hazikutosha,” amesema Tadayo.

Mzee banduka enzi za ujana wake anatajwa kuipenda siasa na kujishughulisha na mambo ya siasa tangu akiwa shule na katika chuo kikuu.

Banduka ambaye ni mzaliwa wa Kijiji cha Mruma, Ugweno , Wilaya ya Mwanga, Mkoani Kilimanjaro amewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya CCM ikiwemo Mjumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa Mkoa wa Kilimanjaro, Mjumbe wa kamati kuu Taifa, Katibu wa CCM Mkoa na baadaye kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa ambapo alihudumu kwa nafasi hiyo katika mikoa mbalimbali hadi alipostaafu.