
Tanga. Viongozi wa taasisi na kampuni binafsi zinazotoa huduma ya usafiri majini mkoani Tanga wametahadharishwa kuwa kama wataendelea kufanya kazi bila kuendana na kasi ya uwekezaji wa Serikali katika bandari ya Tanga, kuna hatari wageni wakachukua nafasi zao.
Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri kwa njia ya maji katika Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac), Nelson Mlali, ametoa angalizo hilo leo Ijumaa, Aprili 18, 2025, wakati wa kikao cha wadau wa usafiri kwa njia ya maji wanaofanya shughuli zao katika Bandari ya Tanga.
Mlali amesema uwekezaji uliofanywa na Serikali katika bandari ya Tanga ni mkubwa, unahitaji watendaji katika kampuni na taasisi binafsi pamoja na za Serikali kutoa huduma kwa kasi kubwa.
Amesema uwekezaji katika Bandari ya Tanga umesababisha idadi ya meli zinazoitumia kupakua shehena kuongezeka kwa kuvuka makadirio.
“Kampuni za watoa huduma zinazodhibitiwa na Tasac lazima ziache kufanya kazi kwa mazoea, badala yake zitii sheria na taratibu zilizowekwa, zishiriki ulinzi na usalama wa rasilimali za nchi, utunzaji wa mazingira ya maji, na kutoa huduma kwa kasi inayohitajika na wateja wote duniani,” amesema Mlali.
Mkurugenzi huyo ametaja baadhi ya changamoto zinazowakabili watoa huduma kwa njia ya maji kuwa ni pamoja na mgongano wa maslahi baina ya mawakala wa forodha dhidi ya mawakala wa meli, watoa huduma ndogondogo dhidi ya mawakala wa meli, mawakala wa meli dhidi ya TPA, na mawakala wa forodha dhidi ya TPA.
Amesema Tasac ilianzishwa chini ya Sheria namba 14 ya mwaka 2017 na kupewa majukumu mbalimbali, likiwamo la udhibiti wa usafiri kwa njia ya maji, ambayo hufanyika kwa kuwasimamia watoa huduma walio katika mnyororo wa usafiri kwa njia ya maji.
Katibu wa Chama cha Mawakala Tanzania (Tafma), Mkoa wa Tanga, Bakari Juma, ameiomba Tasac kuongeza nguvu zake katika Mkoa wa Tanga ili kutoa msukumo zaidi.
“Tunaomba Tasac iongeze msukumo wa utendaji kazi wake Mkoa wa Tanga ili tuendane na kasi ya uwekezaji uliofanywa Tanga,” amesema Bakari.
Hata hivyo, baadhi ya mawakala waliozungumza katika kikao hicho wamesema imekuwa ikijitokeza changamoto ya uhaba wa makontena ya kusafirishia bidhaa ambapo kampuni zinazoshughulikia zimeahidi kuifanyia kazi.