Tanga. Mwili wa Katibu Mkuu wa zamani wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Balozi Juma Mwapachu (82), umezikwa katika makazi yake ya milele, huku viongozi mbalimbali wakimzungumzia.
Balozi Mwapachu alifariki dunia Machi 28, 2025, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam, alikokuwa amelazwa akipatiwa matibabu.

Maziko hayo yamefanyika leo mchana, Machi 30, 2025, katika makaburi ya ukoo wa Mwapachu yaliyopo Kijiji cha Pande, wilayani Tanga. Sala ya mazishi imeongozwa na Sheikh Mohamed Idd.
Akizungumza katika maziko hayo, Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania, Chande Othman, amesema Balozi Mwapachu alikuwa mbunifu wa kuiunganisha Afrika Mashariki anayestahili kuigwa na kuhuisha yale aliyoyaasisi.
Naye Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma maarufu Mwana FA, amesema kuwa Serikali ya Tanzania imempoteza mtumishi bora, hivyo itaendelea kuenzi yote aliyoyaacha.
“Mzee Mwapachu alikuwa kiongozi mchapakazi aliyejali nchi yake, na kwa niaba ya Serikali ya Tanzania tunaahidi kuenzi yote aliyoyaasisi,” amesema Mwinjuma.
Mbunge wa Bumbuli, January Makamba, amemwelezea Balozi Mwapachu kama baba aliyemlea na kumpa miongozo mingi ya namna bora ya kuitumikia nchi na Serikali kwa ujumla.
“Mzee Mwapachu amenilea na kuliongoza kwa mambo mengi juu ya namna bora ya kuitumikia nchi na Serikali kwa ujumla… tumempoteza kiongozi bora na mzalendo wa dhati kwa nchi yake,” amesema Makamba.
Akizungumza wakati wa kuaga mwili wa Mwapachu nyumbani kwake Chumbageni, jijini Tanga, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Dk Abdul Makame, amesema kuwa Balozi Mwapachu alikuwa Katibu Mkuu wa tatu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, lakini kazi alizofanya katika kipindi chake zimekuwa mwongozo hadi sasa.
“Pamoja na kwamba Mwapachu alikuwa Katibu Mkuu wa tatu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, miongozo aliyoiacha imekuwa rejea kwa masuala mengi ya kiutendaji ya Jumuiya yetu,” amesema Dk Makame, ambaye pia ni msaidizi wa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.

Viongozi wengine waliohudhuria maziko hayo ni Kiongozi mstaafu wa ACT-Wazalendo, Zito Kabwe, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba, na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Buriani. Pia walikuwapo makatibu wakuu wa wizara mbalimbali na watumishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.