
Dar es Salaam. Mwanadiplomasia Balozi Juma Mwapachu (82) amefariki dunia leo Machi 28, 2025 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), jijini Dar es Salaam, alikokuwa amelazwa akipatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, mwili wa Balozi Mwapachu utasafirishwa kwenda Kijiji cha Pande, Kiomoni, mkoani Tanga kwa mazishi yanayoarajiwa kufanyika Jumapili Machi 30, 2025.
Kufuatia kifo hicho, Mbunge wa Bumbuli, January Makamba amemzungumzia Balozi Mwapachu kupitia mtandao wa kijamii wa X akiandika:
“Balozi Juma Mwapachu alikuwa mtu mwema aliyekuwa tayari kuwasaidia wenye uhitaji na kuwapa maarifa wale waliotaka kujifunza; alikuwa mtu wa kupendeza, mwenye kicheko rahisi, cha kuambukiza na kilichokuwa na sauti kubwa kiasi. Alikuwa mtu mwenye kujiamini, kutokana na akili yake, upeo wake wa mambo, na misimamo yake iliyojengwa juu ya misingi imara. Alikuwa wa kizazi cha zamani lakini alielewa na kumudu maisha ya kisasa kwa ustadi na kwa urahisi. Hakuwa na aibu wala unafiki katika namna aliyoishi maisha yake na alivyotoa maoni yake. Alijivunia kuwa Mswahili mtaalamu wa lugha ya Kiswahili na mtiifu kwa maadili ya ustaarabu.
Ameongeza: “Alikuwa kielelezo bora cha Mtanzania na adimu miongoni mwa watumishi wa umma aliyelelewa vyema, msomi, msafiri, aliyeelewa misingi ya maisha na mwenye uwezo wa kuzungumza kwa umahiri. Alikuwa msomi wa umma kwa bahati mbaya, si kwa makusudi. Aliishi maisha ya kutosheka yanayostahili kusherehekewa.
“Ameacha alama ile isiyofutika kabisa mioyoni mwa wale aliowagusa na akilini mwa wale aliowafundisha. Leo (Machi 28), amechukua hatua katika safari ambayo sisi sote hatimaye tutaiendea. Roho yake ipumzike kwa amani ya milele. Rambirambi zangu za dhati kwa familia yake.”
Kwa upande wake, Balozi Ami Mpungwe ameandika katika mtandao huo akisema: “Msiba mkubwa wa ndugu yangu, rafiki, mlezi, mwanafamilia na mwenzangu katika utumishi wa kidiplomasia, pamoja na kwenye bodi mbalimbali za umma na binafsi. Kwa wakati wowote ule, kuondoka kwako kungelikuwa mapema mno! Pumzika kwa amani Balozi Juma Mwapachu, maarufu Kaka Juma au JV.”
Wasifu wa Mwapachu
Balozi Juma Mwapachu alizaliwa Septemba 27, 1942 jijini Mwanza, Tanzania.
Alikuwa mwanasiasa na Katibu Mkuu wa zamani wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), nafasi aliyoirithi kutoka kwa Amanya Mushega wa Uganda aliyemaliza kipindi chake cha miaka mitano Machi 24, 2006.
Balozi Mwapachu alipendekezwa kwa nafasi hiyo na Rais wa Tanzania wa wakati huo, Jakaya Kikwete.
Alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa EAC na Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa EAC Aprili 4, 2006.
Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Balozi wa Tanzania mwenye mamlaka kamili na mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco).
Balozi Mwapachu alikuwa mhitimu wa Shahada ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) aliyohitimu mwaka 1969.
Pia alikuwa na Diploma ya Uzamili katika Sheria za Kimataifa, Taasisi za Kimataifa na Diplomasia kutoka Chuo cha India cha Sheria za Kimataifa na Diplomasia kilichopo New Delhi.
UDSM ilimtunuku Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Fasihi mwaka 2005. Pia alipata Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Taifa cha Rwanda.
Balozi Mwapachu alikuwa mwanasheria kitaaluma na alipitia taaluma mbalimbali zikiwamo za benki, maendeleo ya vijijini, diplomasia na sekta binafsi.
Kabla ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa EAC aliwahi kufanya kazi na Wizara ya Serikali za Mitaa na Utawala wa Mikoa katika miaka ya 1970.
Alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa kati ya mwaka 2002 hadi 2006.
Balozi Mwapachu ameshakuwa mwenyekiti wa bodi za wakurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) na za mashirika ya umma ikiwemo Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB).
Alishika wadhifa wa Kamishna wa Tume ya Rais ya Kurekebisha Mashirika ya Umma (PSRC). Alikuwa Mwenyekiti wa Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki.
Aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Biashara ya Nje na Baraza la Uongozi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Balozi Mwapachu aliwahi kuhudumu kama Mjumbe wa Baraza la Uongozi la Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo.
Alihudumu kama mjumbe wa tume mbalimbali zilizoundwa na Rais na alishiriki katika kuandaa Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya 2025.
Balozi Mwapachu aliwahi kujitoa CCM Oktoba, 2015 na kujiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kabla ya kurejea kwenye chama hicho mwaka 2016, ikiwa ni miezi mitano baada ya kujiondoa.