
Balozi mpya wa Kenya nchini Iran amekutana na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kumkabidhi nakala za hati zake za utambulisho.
Kwa mujibu wa taarifa, Jonah Maina Mwangi, balozi mpya wa Jamhuri ya Kenya hapa alikutana jana Jmatatu alasiri na Dkt. Seyed Abbas Araghchi Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuwasilisha nakala za hati zake za utambulisho mwanzoni mwa majukumu yake ya kidiplomasia nchini Iran.
Uhusiano wa Iran na Kenya umekuwa ukiimarika katika miaka ya hivi karibuni.
Ikumbukwe kuwa Shahidi Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Julai mwaka jana alizitembelea nchi tatu za mashariki na kusini mwa bara la Afrika ambazo ni Kenya, Uganda na Zimbabwe kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano na nchi za Afrika. Akiwa Nairobi Shahidi Raisi alikutana na kuzungumza na Rais William Ruto wa nchi hiyo ambapo maafisa wa ngazi za juu wa nchi hizi mbili walitia saini hati 5 muhimu za ushirikiano.