Cape Town. Ebrahim Rasool ambaye ni Balozi wa Afrika Kusini aliyefukuzwa nchini Marekani kutokana na mvutano na utawala wa Rais Donald Trump na utawala wa Serikali yake chini ya Rais Cyril Ramaphosa, amerejea nyumbani na kupokewa kishujaa na umati wa raia wa taifa hilo.
Uamuzi wa Rasool kurejea nyumbani baada ya kufukuzwa Marekani ni mwendelezo wa misimamo yake dhidi ya matamko yanayoashiria ukoloni mambo leo, na kupingana na kauli zinazoashiria msukumo kutoka mataifa ya nje katika utawala wa nchi huru.
Umati wa watu ulijitokeza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Cape Town siku ya Jumapili kumpokea Ebrahim Rasool na mkewe, Rosieda.
Wakati wanawasili walihitaji msaada wa walinzi na polisi ili kupitia ndani ya uwanja wa ndege, baadaye alishika kipaza sauti na kuhutubia umati uliomiminika uwanjani hapo kumpokea.
“Kutangazwa ‘persona non grata’kunakusudia kukudhalilisha. Lakini, unapopokelewa na umati kama huu, kwa upendo kama huu… basi nitavaa hadhi yangu ya ‘persona non grata’ kama alama ya heshima.” Rasool aliwaambia waliokwenda kumpokea kwa kutumia kipaza sauti.

“Haikuwa uamuzi wetu kurudi nyumbani, lakini tunarudi bila majuto,” aliongeza.
Mwezi uliopita, Trump alitoa agizo la kiutendaji la kusitisha misaada yote ya kifedha kwa Afrika Kusini, akidai kuwa Serikali yake inaunga mkono kundi la Kipalestina la Hamas na Iran, na kufuata sera za kibaguzi dhidi ya Wazungu nchini humo.
Afrika Kusini iliwasilisha kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) Desemba 2023, ikiishutumu Israeli kwa kukiuka majukumu yake chini ya Mkataba wa Kuzuia Mauaji ya Kimbari katika vita vyake dhidi ya Ukanda wa Gaza.
Tangu wakati huo, zaidi ya nchi 10 zimejiunga na Afrika Kusini katika kesi hiyo.
“Hatujaja hapa kusema kuwa sisi ni wapinzani wa Marekani. “Hatuko hapa kuwataka muache masilahi yetu na Marekani,” alisema Rasool.
Hizo zilikuwa kauli zake za kwanza hadharani tangu utawala wa Trump kumtangaza ‘persona non grata’ zaidi ya wiki moja iliyopita, kumpokonya kinga na marupurupu ya kidiplomasia, na kumpa hadi Ijumaa kuondoka nchini humo.
Uamuzi wa kufukuzwa Rasool nchini Marekani ulitangazwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, kupitia mtandao wa X, alisema Rasool ni “mwanasiasa anayechochea masuala ya rangi”, anayechukia Marekani na Rais Donald Trump.
Ni jambo nadra sana kwa Marekani kumfukuza balozi wa nchi nyingine.
Chapisho la Rubio lilihusisha habari kutoka tovuti ya kihafidhina ya Breitbart, ambayo iliripoti kuhusu hotuba ya Rasool kwenye wavuti iliyoandaliwa na taasisi ya fikra ya Afrika Kusini.
Katika hotuba yake, Rasool alizungumzia kwa mtazamo wa kitaaluma kuhusu jinsi utawala wa Trump ulivyoshambulia programu za utofauti, usawa na uhamiaji.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.