Balile, Machumu wapita bila kupingwa uchaguzi TEF, wajumbe wapatikana

Songea. Deodatus Balile amechaguliwa bila kupingwa kuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kwa kipindi cha miaka minne ijayo. Uchaguzi huo umefanyika leo, Jumamosi, Aprili 5, 2025, mjini Songea, mkoani Ruvuma.

Balile, ambaye alikuwa mgombea pekee, ameendelea kuaminiwa na wanachama wa jukwaa hilo kuongoza kwa mara ya pili, baada ya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2021.

Pia, Bakari Machumu amechaguliwa tena kuwa Makamu Mwenyekiti wa TEF kwa kipindi cha miaka minne ijayo, baada ya kupita bila kupingwa.

Machumu, ambaye hakuwa na mpinzani katika kinyang’anyiro hicho, ameendelea kupata imani kutoka kwa wanachama wa jukwaa hilo na kuongoza kwa mara ya pili, baada ya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2021.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Frank Sanga amesema kwa mujibu wa sheria na kanuni za uchaguzi TEF, Balile ameshinda kwa kuwa alikuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo na hakuna wapigakura waliopinga.

Kwa mujibu wa sheria na kanuni za uchaguzi za jukwaa hilo, endapo mgombea mmoja tu atajitokeza kwa nafasi yoyote kati ya hizo, atachaguliwa moja kwa moja isipokuwa wanachama watakapoweka pingamizi.

Katika hali hiyo, itabidi kura zipigwe ili kuthibitisha ushindi wake kwa kupata kura zaidi ya nusu.

Pia, amesema kwa mujibu wa sheria na kanuni za uchaguzi za TEF namba 7 na 8, Machumu ameshinda kwa kuwa alikuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo na hakukuwa na wapigakura waliopinga uteuzi wake.

Hii hapa kamati mpya ya utendaji TEF

Wanachama saba wa TEF wamechaguliwa kuwa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya jukwaa hilo. Waliochaguliwa ni Bakari Kimwaga aliyepata kura 114, Salim Salim (108), Joseph Kulangwa (107) na Stella Aron (99).

Wengine waliochaguliwa ni Tausi Mbowe (98), Anna Mwasyoke (83) na Jane Mihanji (73).

Katika kinyang’anyiro hicho, kulikuwa na wagombea 12. Wagombea wengine walikuwa ni Peter Nyanje aliyepata kura 72, Yassin Sadik (60), Reginald Miruko (49), Esther Zelamula (39), na Angelina Akilimali (35).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *