
Dodoma. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi amesema kuwa kuanzia mwaka wa fedha 2025/26, Mfuko wa Mafunzo kwa waandishi wa habari utaanza kutoa msaada wa vifaa vya kisasa kwa waandishi wa habari, ili kuwawezesha kushiriki katika uzalishaji wa maudhui ya ndani yenye ubora na ushindani.
Mfuko huo unasimamiwa na Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari, ambayo ilizinduliwa rasmi Machi 3, 2025 na aliyekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Profesa Palamagamba Kabudi alitoa maelezo hayo leo, Mei 7, 2025, wakati akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Katika bajeti hiyo, Serikali inaomba Bunge liidhinishe jumla ya Sh519.66 bilioni, ambapo kati ya hizo, Sh458.19 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Akiwasilisha bajeti ya wizara yake, Profesa Kabudi amesema kuwa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari tayari imeanzishwa na imeanza kutekeleza majukumu yake, ikiwemo kusimamia maadili ya taaluma ya uandishi wa habari na kuhakikisha weledi katika uandishi wa habari.
Profesa Kabudi ameeleza kuwa bodi hiyo pia inaendesha Mfuko wa Mafunzo kwa Waandishi wa Habari, ambao unalenga kuwajengea uwezo waandishi kupitia mafunzo ya kitaaluma, kusaidia uzalishaji wa maudhui ya ndani, pamoja na kuwezesha tafiti katika nyanja za uandishi wa habari na mawasiliano kwa umma.
“Kwa hiyo, ili kufanikisha malengo hayo, hususan katika eneo la uzalishaji wa maudhui ya ndani, mfuko huu utaanza kusaidia waandishi wa habari kwa kuwapatia vifaa vya kisasa vitakavyowawezesha kushiriki kikamilifu katika utengenezaji wa maudhui bora ya ndani,” amesema Profesa Kabudi.
Profesa Kabudi amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2025/26, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inatarajia kununua kiwanja katika eneo la Mwangaza, Dodoma kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha habari.
Amesema kuwa pamoja na ununuzi huo, wizara itatekeleza hatua ya upembuzi yakinifu wa eneo hilo na kuanza mchakato wa kumpata mkandarasi atakayeendesha ujenzi wa kituo hicho. Kwa ajili ya mradi wa habari kwa umma, jumla ya Sh2.7 bilioni zimetengwa.
Akizungumzia maendeleo ya lugha ya Kiswahili, Profesa Kabudi amesema kuwa kupitia mradi wa kuimarisha Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) na kukibidhaisha Kiswahili, baraza hilo limetengewa Sh3.4 bilioni kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Miongoni mwa shughuli zitakazotekelezwa ni kuboresha mfumo wa kufundishia Kiswahili (Swahili Prime), kusambaza elimu ya Kiswahili kwa makundi maalumu ndani ya nchi kama Wamasai na Wahadzabe, pamoja na uandishi wa Kamusi ya Sheria.
Shughuli nyingine ni usanifishaji mkubwa wa lugha, kuendeleza Kongoo la Kiswahili la Taifa, na kupeleka Kiswahili kimataifa kwa kufungua vituo vya kufundisha lugha hiyo kwa wageni katika nchi 10 duniani.
Wabunge wachangia
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Khadija Hassan Aboud ameshauri wataalamu wa Kiswahili kutafuta maneno ambayo ni mepesi na yanayozungumzika.
“Tujitahidi lugha yetu iwe nyepesi inayoweza kuzungumzika, kusomesheka na kutafsirika kwa wageni, tukiendelea kuyakataa maneno kwa sababu ya kigeni, lugha zote zote zinatohoa maneno kutoka lugha nyingine,”amesema.
Amehoji kuwa watapata wapi maneno kwa vitu vilivyovumbuliwa kama wanakataa kutohoa maneno kutoka katika lugha nyingine.
Khadija amesema kuwa hata Kiswahili chenyewe maneno mengi yametoholewa kutoka kwenye lugha nyingine na kushauri wasiwe wanaongeza maneno magumu ambayo hayawezi kutamkika.
Amesema kwa kufanya hivyo lugha itakuwa ngumu na hivyo watu wanaotaka kujifunza Kiswahili watakimbia kwenda kutafuta wataalamu wa lugha nyingine.
Khadija aliungwa mkono na Mbunge wa Iringa Mjini (CCM), Jesca Msambatavangu ambaye amesema Bakita limekuwa likitengeneza maneno magumu ambayo hayaeleweki kwa Watanzania walio wengi.
“Kwa mfano unatupa neno kishkwambi hadi mtu apate munganiko kuwa ni tablet ndio inayoongelewa inachukua muda, kuna maneno kama kongoo wakati kuna maneno laini na rahisi,”amesema.