Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imeomba bajeti ya Shilingi 519.66 bilioni kwa mwaka wa fedha 2025/2025 ikiwa ni ongezeko la Sh234.36 bilioni katika kiwango cha bajeti kilichoombwa mwaka uliopita wa fedha.
Katika Mwaka uliopita wa fedha, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iliomba kiasi cha Sh285.3 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo.
Akiwasilisha ombi la bajeti hiyo bungeni leo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi amesema kuwa kipaumbele kikubwa katika bajeti hiyo ni ujenzi wa viwanja na ukarabati wa miundombinu kwa ajili ya kuwezesha uandaaji wa Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN) 2025 na Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 zilizopangwa kufanyika Tanzania, Kenya na Uganda.
“Katika kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika kwa ufanisi mkubwa, Serikali kupitia Wizara imeendelea na ujenzi na 90 ukarabati wa miundombinu mbalimbali ya michezo ikiwamo ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa na Uhuru na ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu wa Arusha na Dodoma.

“Aidha, Serikali inaendelea na ukarabati na ujenzi wa viwanja vitano vya mazoezi
vitakavyotumika wakati wa michuano hiyo vilivyopo jijini Dar es Salaam. Serikali pia imejipanga kujenga viwanja vingine vitano (5) vya mazoezi kwa ajili ya maandalizi ya AFCON 2027 jijini Arusha,” amesema Waziri Kabudi.
Ikumbukwe kwa sasa, serikali inajenga uwanja wa kisasa wa soka jijini Arusha ambao utaingiza watazamaji 32,000 wenye thamani ya Sh286 bilioni na pia inajenga mwingine jijini Dodoma kwa gharama ya Sh350 bilioni.
Maeneo mengine ambayo Kabudi amesema yatapewa kipaumbele ni ya masuala ya habari, utamaduni na sanaa.
“Malengo yaliyopangwa kutekelezwa ni kufanya utafiti wa urithi wa utamaduni usioshikika pamoja na kuandaa Atlasi ya Lugha za Jamii na Atlasi ya Tamaduni Mbalimbali za Makabila ya
Tanzania, kuhuisha Sera ya Utamaduni ya mwaka 1997; kuratibu uandaaji wa mkakati wa kitaifa wa kukabiliana na mmomonyoko wa maadili nchini; kuendesha Tamasha 119 la Nne la Utamaduni la Kitaifa.
“Kuratibu Matamasha ya utamaduni yanayoandaliwa na wadau; kuratibu ukuzaji na uendelezaji wa lugha ya Kiswahili kitaifa na kimataifa; kuratibu Maadhimisho ya Nne ya Kitaifa na Kikanda ya Siku ya Kiswahili Duniani pamoja na makongamano ya Kiswahili ya wadau na kuratibu kikaokazi cha Maafisa Utamaduni nchini,” amesema Profesa Kabudi.