
SAKATA la wachezaji watatu wa kigeni waliobadilisha uraia wao limechukua sura mpya baada ya wawili kati yao kuanzishwa katika kikosi cha timu ya Singida Black Stars dhidi ya Kagera Sugar.
Katika kikosi ambacho Singida imekiweka hadharani mchana huu kitakachocheza dhidi ya Kagera Sugar kimewajumuisha wachezaji wawili hao kati ya watatu ambao ni kiungo Damaro Camara na Arthur Bada.
Bada raia wa Ivory Coast na Damaro kutoka Guinea watacheza mchezo huo wa kwanza wakiwa raia wa Tanzania huku Emannuel Keyekeh akikosekana kwenye mchezo huo.
Kwenye kikosi hicho cha leo Singida imeanza na wachezaji 12 wa kigeni wanaohitajika kikanuni, ingawa wachezaji wengine watatu Ibrahim Imoro, Keyekeh na kipa Amas Abasogie wametupwa jukwaani.
Singida ambayo inacheza mchezo wake wa kwanza wa ligi ndani ya mwaka 2025 ikiwa nyumbani imeanza na kipa Metacha Mnata, mabeki wakiwa Ande Koffi, Nahodha Charles Manyama, Ernest Malonga, Antony Tra BI Tra.
Viungo walioanzishwa kwenye mchezo huo ni pamoja na Damaro, Morice Chukwu, Marouf Tchakei wakati washambuliaji wakiwa Elvis Rupia, Bada na Jonathan Sowah.
Kwenye benchi wamo, Hussein Masalanga, Frank Assinki, Kennedy Juma, Ayoub Lyanga, Serge Pokou, Eliuter Mpepo, Kelvin Nashon, Victor Adebayor na Makoye NA Athuman waliotoka kikosi cha timu ya vijana.
Katika mechi hiyo, mapema tu katika dakika ya sita, nyota mpya Jonathan Sowah aliyewahi kutakiwa na Yanga na Simba, amewaka chuma ya kwanza akiitanguliza Singida Black Stars.