Baba aliyemuua mwanawe kisa kuchelewa kutembea, jela miaka 15

Geita. Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Geita, imemuhukumu kifungo cha miaka 15 jela, Imani Salehe (23) baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mtoto wake mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu.

Hukumu hiyo imetolewa leo Aprili 30, 2025 na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Calvin Mhina, baada ya mshtakiwa kukiri kosa la kumuua mtoto wake Monica Imani, bila kukusudia.

Kesi hiyo iliwasilishwa kwa ajili ya kusomewa hoja za awali, lakini Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Kabula Benjamin ameiomba Mahakama kubadilisha hati ya mashitaka kutoka kuua kwa kukusudia na kuwa kuua bila kukusudia, kinyume na Kifungu cha 195 na 198 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Imani Salehe (23) aliyehukumiwa kifungo cha miaka 15 jela kwa kosa la kumuua bila kukusudia mtoto wake mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu kwa sababu za kuchelewa kutembea.

Akiwasilisha maelezo ya kosa, Wakili Kabula amesema tukio hilo lilitokea Septemba 17, 2024 huko Chato, mkoani Geita, Salehe alimuua mtoto wake Monica kwa kumyonga shingoni, kwa madai kwamba mtoto huyo alikuwa amechelewa kutembea, jambo lililomkwaza baba yake.

Ripoti ya uchunguzi wa kifo hicho ilibaini kuwa chanzo cha kifo kilikuwa ni kukosa hewa baada ya kunyongwa.

Baada ya kukiri kosa la kuua bila kukusudia, Mahakama ilimkuta mshtakiwa na hatia chini ya Kifungu cha 195 na 198 cha Kanuni ya Adhabu.

Upande wa mashitaka uliwasilisha vielelezo vitatu; ripoti ya uchunguzi wa kifo, ramani ya eneo la tukio na maelezo ya onyo ya mshtakiwa.

Jengo la Mahakama kuu masjala ndogo ya Geita

Wakili wa Serikali aliomba Mahakama kutoa adhabu kali, akieleza kuwa mshtakiwa amemuua mtoto asiye na hatia na kuchelewa kutembea, si kosa.

Aidha, ameieleza Mahakama kuwa mshtakiwa amekatisha ndoto za mtoto ambaye alikuwa ni sehemu ya kizazi cha baadaye cha Taifa.

Wakili wa utetezi, Yesse Lubanda aliiomba Mahakama imuhurumie mshtakiwa kwa kuwa ni kosa lake la kwanza, ana umri mdogo wa miaka 23, na bado ni sehemu ya nguvu kazi ya Taifa. Aliongeza kuwa mshtakiwa anawalea wadogo zake watatu na ana mke anayemtegemea, huku mama yao akiwa mzee.

Jaji Mhina amesema kutokana na hoja za pande zote mbili na aina ya kosa lililotendwa, ni wazi kuwa kushindwa kutembea kwa mtoto halikuwa kosa na kifo hicho kingeweza kuzuilika.

Hivyo, alimuhukumu mshtakiwa kutumikia kifungo cha miaka 15 jela na akaeleza kama hajaridhika na hukumu hiyo, ana haki ya kukata rufaa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *