
Mwanza. Ikiwa imepita miezi minne tangu Mwananchi iripoti habari kuhusu baadhi ya wanachama wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) Mkoa wa Mwanza kutishia kufanya maandamano hadi Ofisi ya Jaji Mfawidhi wa Mkoa wa Mwanza kama ombi lao la kuitishwa uchaguzi wa kujaza nafasi za viongozi waliojiuzulu halitazingatiwa, hatimaye uchaguzi huo umefanyika na viongozi wapya wamepatikana.
Mawakili hao 46 walijaza majina na kusaini fomu maalumu ya kushinikiza uongozi wa TLS ngazi ya Taifa kuitisha uchaguzi wa kujaza nafasi za viongozi walioandika barua ya kujiuzulu jambo ambalo Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi aliahidi kulifanyia kazi kwa mujibu wa sheria.
Miezi minne baadaye, TLS Mwanza wameitisha uchaguzi huo jana Jumatano ambapo miongoni mwa viongozi waliochaguliwa ni pamoja na Mwenyekiti wa TLS Mkoa wa Mwanza, Joseph Mugabe ambaye amewashinda, Gibson Ishengoma, Lugano Kitangalala, Egbert Mujungu na Amos Gondo.
Katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa TLS Mkoa wa Mwanza, Wakili Erick Mutta aliibuka mshindi akimgalagaza, Esther Tuvave, Stella Sangawe na Duttu Chebwa huku nafasi ya Ofisa Masurufu, Godfrey Basasingohe aliibuka kidedea mbele ya Inhard Mushongi na Ernest Muhagama.
Katika nafasi za mwakilishi wa TLS Mkoa wa Mwanza katika Mkutano Mkuu (AGM), Sekundi Sekundi alipigiwa kura ya “Ndiyo” kutokana na kuwa mgombea pekee, huku Mokami Robi akichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu itakayoundwa.
Akizungumza baada ya uchaguzi huo, Mwenyekiti mpya wa TLS Mwanza, Joseph Mugabe alisema kipaumbele chake ni kushughulikia changamoto ya mpasuko miongoni wa wanachama wa TLS Mwanza uliosababishwa na kukosekana uongozi thabiti kwa muda mrefu.
“Nimekuwa Wakili Mwanza kwa miaka zaidi ya 10 changamoto kuu iliyopo hapa ni uwepo wa malalamiko yanayojirudia bila kushughulikiwa. Miongoni mwake ni chama hicho kukosa ofisi ya kueleweka mkoani humo, ninaenda kuweka mwonekano mzuri wa uongozi.”
“Kamati za chama hazifanyi kazi kwa muda mrefu, ninaamini nikiwa na jopo langu tunaenda kuunda upya uongozi wa TLS Mwanza ikawe ya mfano itakayoleta mageuzi hadi ngazi ya taifa,” amesema Mugabe.
Ofisa Masurufu wa TLS Mkoa wa Mwanza, Godfrey Basasingohe alisema suala la kwanza kulishughulikia ni usimamizi wa mapato na fedha zinazotolewa na wanachama na kuhakikisha zinawanufaisha wanachama na siyo watu wasiyohusika.
“Tunaamini kuanzia sasa hakutakuwa na makosa ya rasilimali za TLS Mwanza kutumiwa na watu ambao siyo wanasheria wa Mwanza. Tutahakikisha kila mwanachama wa TLS anafurahia kesi ya TLS kutokana na ushiriki wake kikamilifu katika shughuli za chama sambamba na kuisaidia jamii yetu,” amesema Basasingohe.
Makamu Mwenyekiti wa TLS Mwanza, Erick Mutta amewataka mawakili wa Mwanza na wasiyo mawakili kutegemea uongozi ambao utasimamia na kutetea haki zao na za jamii sambamba na weledi katika taaluma ya uwakili nchini.
Hata hivyo, Wakili Esther Tuvave aliyekuwa anagombea nafasi ya makamu mwenyekiti aliyoshinda Mutta, alipoulizwa kuhusiana na uchaguzi huo alikiri kushindwa kihalali huku akisema anaamini waliochaguliwa kuongoza chama katika mkoa huo wataleta mageuzi.
“Pamoja na kuwa nimeshindwa kwenye boksi la kura ila naamini hawa waliochaguliwa wote ni majembe na watatuwakilisha vyema kwenye uongozi huo. Tutawapatia ushirikiano wa kutosha ili watuletee mabadiliko na kutatua changamoto tunazopitia,” amesema Tuvave.
Awali nafasi hizo zilikuwa zinashikiliwa na viongozi waliojiuzulu ambao ni Msafiri Henga (aliyekuwa Mwenyekiti wa TLS Mkoa wa Mwanza), Marina Mashimba (Makamu Mwenyekiti) na Angelo Nyaoro (Ofisa Masurufu).