Mufindi. Baada ya zaidi ya miaka 10 ya kuishi bila huduma ya umeme, wakazi wa Kitongoji cha Ilala, Kijiji cha Nyololo Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa, hatimaye wameunganishiwa nishati hiyo kupitia Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini (Rea), hatua iliyowapa matumaini mapya ya maendeleo na kuboresha maisha yao.
Huduma hiyo imeanza kutolewa baada ya uwekaji wa jiwe la msingi la mradi huo uliofanyika Mei 2, 2025 katika kitongoji hicho, hafla iliyowahusisha viongozi wa Serikali na wakazi wa eneo hilo.
Mradi huo ni miongoni mwa miradi tisa yenye thamani ya Sh20.4 bilioni iliyokaguliwa na kuzinduliwa wakati wa mbio za Mwenge katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Serikali kusukuma mbele gurudumu la maendeleo vijijini.
Wakizungumza wakati wa hafla hiyo, baadhi ya wakazi akiwamo Zedeck Hamisi na Winfrida Sanga wamesema ujio wa umeme umeleta matumaini mapya na utasaidia kuchochea shughuli za maendeleo na kuinua hali ya kiuchumi ya jamii hiyo.
“Tumeishi gizani kwa zaidi ya miaka kumi. Tulilazimika kwenda maeneo ya mbali kutafuta huduma ya umeme. Leo tuna matumaini kwamba nyumba zetu zitapata mwanga na shughuli zetu za kiuchumi zitaimarika,” amesema Hamisi.
Aidha, Hamisi amesema umeme huo utasaidia kuwapa vijana sababu ya kubaki vijijini na kushiriki katika shughuli za uzalishaji badala ya kuhamia mijini kutafuta ajira.
“Vijana sasa wataweza kuanzisha shughuli kama useremala, ushonaji na uchomeleaji vyuma. Hii itasaidia kuongeza kipato na kuboresha maisha yetu,” ameongeza.

Kwa upande wake, Meneja wa Tanesco Wilaya ya Mufindi, Modest Mahururu, amesema mradi huo unalenga kupeleka umeme katika vitongoji 107 wilayani humo. Hadi sasa, vitongoji 30 tayari vimeunganishwa na kazi inaendelea katika vitongoji vingine 40.
“Mradi huu si tu kwamba utaongeza fursa za biashara vijijini, bali pia utapunguza gharama za ujenzi kupitia huduma kama uchomeleaji wa vyuma kwa gharama nafuu,” amesema Mahururu.
Amesema kuwa huduma ya umeme pia imeboresha mawasiliano kwa kuwa wakazi sasa wanaweza kuchaji simu zao muda wote, tofauti na zamani ambapo walilazimika kutafuta huduma hiyo mbali na makazi yao.
Kwa mujibu wa Mahururu, mradi huo unakadiriwa kugharimu Sh17 bilioni, fedha zilizotolewa na Serikali kupitia Rea.
Akizungumza kwa niaba ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Aziz Aboubakar ameipongeza Rea kwa kazi kubwa ya kuhakikisha maeneo ya vijijini yanafikishiwa huduma ya umeme.
“Niwapongeze Rea kwa juhudi kubwa wanazofanya kusogeza huduma ya nishati kwa wananchi. Pia tunawashukuru viongozi wa Halmashauri ya Mufindi kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo,” amesema Aboubakar.