Baada ya ‘mauaji ya halaiki’ ya Jabalia, Israel yaua Wapalestina 38 wa familia moja Khan Yunis, wamo watoto 14

Jeshi la utawala haramu wa Kizaayuni wa Israel limeshambulia mji wa Khan Younis na kuua Wapalestina 38 wa familia moja, wakiwemo watoto 14.

Mauaji hayo ya leo yanafuatia mauaji ya usiku wa kuamkia leo, ambapo zaidi ya Wapalestina 150 waliuawa shahidi na kujeruhiwa katika mashambulizi ya kinyama na kikatili yaliyofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kwenye kambi ya wakimbizi ya Jabalia katika Ukanda wa Ghaza, katika kile Shirika la Ulinzi la Raia la Palestina limekielezea kuwa ni “mauaji makubwa ya halaiki”.

Taarifa hiyo iliyotolewa na shirika hilo imefichua kuwa wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wameripua majengo 12 ya makazi ya raia katika eneo la al-Hawaja kwenye kambi hiyo iliyozingirwa.

“Raia wanatoa miito kwa hofu na wasiwasi mkubwa wakitaka kuelekea mahali pa matukio ili kusaidia kuwaondoa majeruhi,” imeeleza taarifa hiyo, ikisisitiza haja ya haraka ya msaada baada ya shambulio hilo.

Kambi ya wakimbizi Wapalestina ya Jabalia iliyoko kaskazini mwa Ghaza, imekuwa moja ya maeneo yaliyoathirika zaidi katika vita vya kinyama vinavyoendelezwa na utawala haramu wa Israel, huku ikiandamawa na mashambulizi ya angani na ardhini.

Taarifa hiyo Shirika la Ulinzi la Raia la Palestina imeongeza kuwa jeshi la Kizayuni limelenga nyumba za familia za Najjar, Abu Al-Ouf, Salman, Hijazi, Abu Al-Qumsan, Aqel Abu Rashid, Abu Al-Tarabish, Zaqoul, na Shaalan.

Kubomolewa kwa majengo ya makazi ya watu na kuongezeka idadi ya vifo vya raia kumezidisha hali mbaya ya kibinadamu huko Jabalia, huku hospitali za eneo hilo zikielemewa na kushindwa kutoa huduma za matibabu kwa majeruhi.

Hayo yanajiri huku idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi katika vita vya kikatili na mauaji ya kimbari yanayofanywa na jeshi la utawala ghasibu wa Israel katika Ukanda wa Ghaza tangu Oktoba mwaka jana ikiwa inakaribia 43,000…/